24 February 2011

RC adai waandishi hawana msaada Gongolamboto

Gladness Mboma, Peter Mwenda

KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Sadiq amewatolea maneno ya dharau waandishi wa habari na kudai kwamba hawana msaada
wowote kwa waathirika wa mabomu ya Gongolamboto.

Bw. Sadiq alisema hayo baada ya kuchukizwa na kitendo cha waandishi wa habari kumhoji mwathirika wa mabomu, Bi. Zaina Kilo na mjukuu wake Tizo Bisona ambao walifika katika Ofisi za Serikali za Mitaa Ukonga kulalamikia kukosa huduma tangu waruhusiwe hospitali ya Muhimbili na Amana.

"Sasa wewe mama, umetufuata sisi au waandishi wa wabari? Wamekuoji wamekupa nini hakuna aliyekuja na unga wala mchele, sana sana wao ndio watakaofaidika kwa kuonesha picha yako na ya mjukuu wako kwenye runinga, magazeti na kwenye mabango," alisema.

Aliendelea kumfokea mama huyo mbele ya waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Suleiman Kova na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maafa.

Bw. Sadiq aliendelea kusema kuwa habari hiyo aliyoitoa kwa waandishi wa habari itaripotiwa tofauti na kuonekana kwamba kamati nzima haijatenda mambo mema yaliyojitokeza kwa waathirika wa mabomu.

Kitendo hicho kilichofanywa na Bw. Sadiq kilimfanya mama huyo kuangua kilio mbele ya watu waliokuwepo, hali iliyomfanya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Leonadis Gama kwenda kumuondoa pale na kumwingiza ndani.

Awali akitoa malalamiko hayo kwa waandishi wa habari, Mama huyo alisema kuwa mjukuu wake alijeruhiwa kichwani na mgongoni na kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kushonwa nyuzi 10 na yeye kulazwa katika Hospitali ya Amana.

Alisema kuwa wakati tathmini inapita, yeye pamoja na mjukuu wake walikuwa bado wamelazwa hospitalini na waliporuhusiwa na kwenda kutoa malalamiko yao Serikali za Mitaa hawakupata ushirikiano.

"Tulipoenda Serikali za Mitaa walituambia kwamba wanaoshughulikiwa ni wale ambao nyumba zao zimebomoka na kwamba tahmini imekwishafanywa," alisema.

Alisema kuwa kutokana na majibu hayo waliamua kwenda katika kitengo hicho cha maafa kwa ajili ya kuomba msaada.

"Pale karibu na nyumba yangu kuna majirani zangu nyumba zao zilipitiwa na mabomu, lakini hawakujeruhiwa kama sisi na wanakwenda kazini kama kawaida, lakini wanapelekewa msaada wa vyakula na vitu vingine. Lakini mimi na mjukuu wangu ambao tumejeruhiwa, tunayumbishwa na kuambiwa kwamba tathmini imekwishapita, kweli hii ni haki," alihoji.

Waandishi wa wabari walichukizwa na kitendo cha kubezwa kwamba hawana msaada kwa waathirika na kuinuka vitini walipokuwa wameketi na kusambaa, ndipo Kamanda Kova alipoingilia kati kutafuta suluhu.

Baadaye, Bw. Sadiq aliwafuata waandishi wa habari na kuomba radhi kwamba ameteleza na kwamba bila wao yote yaliyofanyika baada ya kutokea milipuko ya bomu yasingewezekana.

5 comments:

  1. CCM wote ni kama mbwa koko. Sasa huyu na Mary Chatanda kuna tofauti. Kweli kunguru hafugiki

    ReplyDelete
  2. Huu ni upuuzi mtupu? ccm inaingiaje katika hili? na nyie waandishi ujumbe umefika,m mnashindwa hata bkuchangishana kutoa msaada? ila kazi kulewa ofa tu na kuchukua mishiko ya maafa, huu si uungwana. Hongera RC. waandishi wa siku hizi si wakuachiwa,nao wapewe za uso kama hivyo, umekosea kuomba radhi.

    ReplyDelete
  3. Saafi saana, waandishi wanaipeleka nchi hiim pabaya.

    ReplyDelete
  4. Mhhh..kweli hapo ndio ujue kwa nini TZ hatuwezi kupata maendeleo..Viongozi kama hawa tunategemea nini??
    Bibi wa watu keshahangaika serikali za mitaa bila kusaidiwa, kaamua bora aeleze ukweli kwa waandishi..na kila mtu anajua ukweli unauma..
    Unaweza kukuta hata hapo kwenye ofisi ya waathirika, hakuna aliyekuwa anamjali mpaka alipoongea na waandishi wa habari..
    Badala ya huyo kaimu wa mkoa kuonyesha uzalendo wake, analeta ubabe..Utaachaje kuilaumu CCM wakati huyu kateuliwa na serikali ya CCM??
    Mungu ibariki Tanzania
    Kachala

    ReplyDelete
  5. Watanzania wengi nchi yetu bado hamjaifahamu, kunapotokea maafa watu wengi mnaonglea kuchangia tu. Naomba mnijibu swali hili, Hivi ninyi mnajua bajeti ya maafa Tanzania kwa mwaka ni shiringi ngapi? na inatumikaje? Bajeti ya maafa kila mwaka inapangwa, na maafa yasipotokea inachakachuliwa, maafa yakitokea watu wachange, huo ni upuuzi. ningefurahi kama watu wangeibana serikali iwe bajeti peupe kabala ya kuchangia. hata hivyo serikali ndo imesababisha maafa ni wajibu wake kulipa. hivi wewe ukisababisha ajari serikali inakusaidia kulipa?
    Waandishi wa Habari siyo kazi yao kuchangisha, kazi yao ni kutoa taarifa sahihi. Aliye walaumu waandishi wa habari uelewa wake ni mdogo.

    Serikalika, inatakiwa ibanwe ilipe hao watu sawa, sawa, Mbona dowans hamsemi tuchangie. Dowans na waathirika wa Mabomu yote ni madeni tu yaliyosababishwa na serikali.

    ReplyDelete