Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari jana imezindua mashindano ya kuchoma nyama 'Safari Lager Nyama Choma 2011' na kutangaza
zawadi za washindi ambapo bar itakayoibuka bingwa itanyakua sh. milioni.
Baa itakayokuwa ya pili katika mashindano hayo itapewa sh. 800,000, wa tatu sh. 600,000, wa nne sh. 400,000 na wa tano sh. 200,000. Zawadi hizo zimegawanywa katika kila mkoa.
Akizungumza Dar es Salaam jana Meneja wa bia ya Safari Lager, Fimbo Butallah alisema mashindano ya mwaka huu yatafanyika katika mikoa minne ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Mbeya ambao umeongezwa mwaka huu.
Butallah alisema utaratibu wa mashindano hayo, yataendeshwa kwa njia ya simu ambapo wananchi watatakiwa kutuma ujumbe wa maneno 'Safari kisha mkoa ikifuatiwa na jina la baa' kwenda namba 15540.
"Mashindano haya hushirikisha majiko ya baa mbalimbali katika umahiri wa kuchoma nyama na hatimaye zawadi hutolewa kwa washindi,' alisema Butallah.
Alisema madhumuni makubwa ya bia ya Safari ni kuendesha mashindano hayo, ambayo yamekuwa kivutio kwa walaji wa nyama na watumiaji wa bia hiyo ni kuleta changamoto kwa majiko yanayochoma nyama ili kuhakikisha walaji wanapata kilichobora.
Meneja huyo alisema vigezo vitakavyotumiwa na majaji wa mashindano hayo ni usafi wa eneo, vifaa na muhusika, nyama inavyosafishwa na maji, uchaguzi wa nyama, maandalizi, uchomaji, muda, ladha na nyama inavyopelekwa kwa mlaji.
"Baa zitakazofanikiwa kuingia katika kinyang'anyiro hicho zitapewa semina elekezi juu ya vigezo hivi kabla ya mpambano," alisema Butallah.
No comments:
Post a Comment