01 February 2011

Zanzibar Ocean View yabanwa mbavu

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

WAWAKILISHI wa Zanzibar kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Zanzibar Ocean View wameshindwa kuutumia vyema
uwanja wao wa nyumbani, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na AS Vital Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), katika mechi iliyochezwa juzi Uwanja wa Amaan saa 2 usiku.

Katika mechi hiyo, tizo zilikianza kipindi cha kwanza kwa nguvu huku kila moja ikitaka kupata mabao lakini hata hivyo mabeki wa pande zote walikaa imara kuondoa hatari.

Mabao yote yaliingia kipindi cha pili, baada ya miamba hiyo kwenda mapimziko wakiwa hawajafungana.

Wageni Vital, ndiyo iliyoanza kutangulia kupata bao la kuongoza katika dakika ya 72, kupitia kwa mchezaji Mfungungu Afred ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukuwa nafasi ya Ibara Franchee, baada ya
kupokea pasi safi kutoka kwa Romarik Rogombe.

Kuinga kwa bao hilo kulizidisha kasi ya mashambulizi kwa pande zote
mbili, ambapo dakika ya 82 Othman Tamim wa Zanzibar Ocean aliikosesha timu yake bao la wazi.

Jitihada za Zanzibar Ocean View kutaka kusawazisha bao hilo zilizaa matunda dakika moja kabla ya mwamuzi kupuliza kipyenga cha kumaliza mpira ambapo Kheir Salum alitumbukiza mpira kimiani na kuzifanya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Kutokana na matokeo hayo Zanzibar Ocean sasa inatakiwa kutoka na ushindi wa bao 1-0 au zaidi katika mchezo wa marudiano utakaofanyika nchini Congo wiki mbili zijazo.

No comments:

Post a Comment