01 February 2011

Wasanii watakiwa kujifunza kingereza

Na Addolph Bruno

WASANII wa sanaa za maonesho na filamu nchini wametakiwa kuongeza bidii kujifunza lugha ya kiingereza, waweze kupanua wigo wa soko la kazi zao
kimataifa.

Mwito huo ulitolewa Dar es Salaam jana na msanii maarufu wa maigizo nchini Christina Inocent 'Mama Bishanga', alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya sanaa hapa nchini.

Mama Bishanga ambaye kwa sasa anasomea shahada ya shughuli za kijamii nchini Marekani, alisema kazi za sanaa za Tanzania hazionekani katika nchi za nje hususani Marekani ikilinganishwa na kazi za nchi nyingine ambazo kutokana na tatizo la lugha.

"Kazi za wasanii wa nchi zote duniani zinatumika sana nchini Marekani, watu wananunua lakini nimefanya utafiti nimeona kazi za hapa kwetu nazo zipo kule lakini hazina soko," alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo wasanii hawana budi kukubali kuingia darasani kujifunza lugha ya kiingereza, bila kupoteza nafasi ya lugha ya kiswahili katika sanaa.

Mbali na hilo Mama Bishanga ambaye ni msanii wa zamani wa kundi la Kaole, alisema anaipongeza Serikali ya awamu ya nne kwa kusaidia michezo na kuomba iongeze juhudi iwasaidie wasanii wa sanaa za maonesho, ambao kazi zao zina soko kubwa kimataifa.

Hata hivyo Mama Bishanga alisema hali ya sanaa hapa nchini imefikia hatua nzuri, amewapongeza wasanii kwa juhudi wanazozionesha na kuwataka kuzingatia maadili.

1 comment:

  1. SIO LAZIMA WASANII KUJUA KIINGEREZA. WATANZANIA TUTAJUA LINI KUIENZI LUGHA YETU? HIVI FILAMU ZA KIHINDI, KIJAPAN, KIGIRIKI, KIRENO, KIFILIPINO NA NYINGINE NYINGI ZINAUZIKAJE?
    TATIZO LILILOPO KWA KIWANDA CHA SANAA HIZI ZA MAIGIZO NI WATU KUNG'ANG'ANIA KUFANYA KAZI ZOTE WENYEWE. MTUANATAKA AWE PRODUCER, AWE DIRECTOR, AWE MUIGIZAJI, AANDIKE SCRIPT, AANDIKE HATA SUBTITLE, WAKATI KIINGEREZA CHENYEWE CHA NGUMBALU. HAPO NDIPO WANAPOHARIBU.
    KWA NINI USIFANYE KILE TU UNACHOWEZA, NA USICHOWEZA MPE ANAYEWEZA KUKUSAIDIA? WAPO WATU AMBAO WAKO TAYARI HATA KUSAIDIA BURE KWA MFANO, KUTAFSIRI SCRIPT, AU KUANDIKA SUBTITLES, LAKINI " MASTAA " HILO HAWATAKI. KWAO KUONEKANA MAJINA YAO YAKIJIRUDIARUDIA KWENYE TITLES NDIYO FURAHA YAO. NAMNA HII WATAUZA WAPI? HATA ZIMBABWE TU HATAPATA SOKO, NINI ULAYA.
    UKISOMA SUBTITLE, AU VIBWAGIZO VYA KIINGEREZA KWENYE FILAMU NYINGI ZA KIBONGO NI AIBU. MANENO YANAYOZUNGUMZWA NA WAIGIZAJI HAYAENDANI KABISA NA TAFSIRI YA KIINGEREZA ILIYOTOLEWA, WAKATI MWINGI INAPOTOSHA MAANA KABISA. HEBU SOMA HII, " HUYU NI MAMA YANGU MZAZI..." KWA KIINGEREZA, " THAT IS MOTHER IAM BIRTH WITH..." KWA YEYOTE MWENYE AKILI, TAFSIRI HII HAITAVUTIA MTU ASIYEJUA KIINGEREZA KUNUNUA MKANDA HUO. SIYO KWA SABABU MUIGIZAJI HAJUI KIINGEREZA, ILA NI KWA SABABU YA UBINAFSI TU.

    ReplyDelete