25 January 2011

Serikali yafagilia kozi ya FIFA

Na Zahoro Mlanzi

SERIKALI imeifagilia kozi inayoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ya uandaaji wa matukio iliyofungiliwa jana, Dar es Salaam.
Programu hiyo imeingizwa katika kalenda ya FIFA mwaka huu na ilizinduliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni Vijana na Michezo, Emmanuel Nchimbi ambayo inashirikisha Makatibu wa klabu, Mameneja wa Uwanja na Wadhamini wa soka.

Kabla hajafungua kozi hiyo, Nchimbi aliizungumzia program hiyo baada ya kupata muktasari kutoka kwa Ofisa Maendeleo wa FIFA, Ashford Mamelod juu kozi hiyo na kusema itafungua njia ya kutatua migogoro ya mara kwa mara ndani ya klabu nchini.

"Siku zote serikali itaendelea kujipanga kuinua soka na kama baada ya kozi hiyo timu zikijipanga vizuri katika kuandaa matukio kama michezo ya kirafiki, Ligi Kuu na mingine hakika mapato yatakuwa makubwa," alisema Nchimbi.

Alisema mafunzo yatakayotolewa ni lazima yafanyiwe kazi na si kuyaacha katika mabegi yao waliyokuja nayo, kama vitendo vitafanyika hakika migogoro haitakuwepo kwani kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.

Waziri huyo alisema kutokuwa na elimu ya uandaaji wa matukio ndiyo chanzo cha migogoro inayotokea katika klabu mbalimbali nchini, lakini aliongeza kozi hiyo itasaidia kuondoa migogoro hiyo.

Kabla ya Nchimbi kuzungumza, Mamelod alielezea juu ya umuhimu wa kozi hiyo, ambapo alisema itasaidia klabu kuandaa mechi vizuri huku zikijua usalama wa mashabiki, tiketi na mambo mengine yanayohusu mechi jinsi inavyotakiwa kuandaliwa.

Alisema kozi hiyo ndiyo imezinduliwa kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam na sasa itaendelea kufanyika katika nchi wanachama wa FIFA na kwamba ana imani Tanzania, itakuwa ya kwanza kupata maendeleo ya soka kupitia programu hiyo.

Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga aliishukuru FIFA kwa kuleta kozi hiyo kwa mara ya kwanza nchini na kwamba itasaidia kuzikomboa klabu katika janga la kupata mapato madogo.

No comments:

Post a Comment