27 January 2011

Wasichana watesa form IV

Wa Kwanza: "Siamini kabisaa, ila Mungu alikuwa akiniona nikisoma kwa bidii. Nimepata nguvu kubwa ya kuendelea kusoma kidato cha tano na sita na chuo kikuu. Matarajio yangu ni kuwa daktari," alisema kwa furaha Lucylight.

Wa Pili:
"Siri ni ufuatiliaji wa karibu wa walimu na Meneja wa shule. Pia kujituma mimi mwenyewe, mazingira mazuri ya shule na uhamasishaji wa wazazi wangu, lakini pia siwezi nikasahau msaada wa sala," alisema Maria-Dorin.

Na Waandishi Wetu, Dar, Arusha

WASICHANA wameendelea kuonesha makali yao katika masomo dhidi ya
wavulana baada ya kushika nafasi nane bora kati ya 10 kitaifa kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa jana.

Matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Joyce Ndalichako jana Dar es Salaam, yanaonesha kuwa nafasi ya kwanza hadi ya sita zimechukuliwa na wasichana, wakifuatiwa na wavulana wawili (namba 7 na 8), kisha mabinti hayo kumalizia nambari tisa na 10.

Kutokana na matokeo hayo, wanafunzi wawili walioongoza kitaifa walielezea furaha hao walipozungumza na Majira kwa nyakati tofauti, wakisema siri ya mafanikio yao ni kujituma wenyewe, juhudi za walimu wao, mazingira mazuri ya shule pamoja na msukumo wa wazazi wao.

Akizungumza na Majira Tengeru mkoani Arusha, mwanafunzi wa kwanza kitaifa kutoka Shule ya Sekondari ya wasichana Marian, Bi. Lucylight Mallya alisema matokeo hayo yamempa moyo na kumjaza nguvu ya kuongeza bidii kwa masomo yanayokuja ya kidato cha tano na ya chuo kikuu.

Kwa upande wake Maria Dorin Shayo aliyeibuka wa pili, pia kutoka shule hiyo, ametoboa siri ya suhindi wake ni kuwa mazingira mazuri ya shule na kupata walimu wa kutosha na wenye sifa.

Pamoja na washidni hao watahiniwa wengine katika kumi bora kitaifa ni, Sherryen Mutoka wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Barbro-Johansson, (Dar es Salaam), Diana Matabwa, St. Francis Girls (Mbeya) na Neema Kafwimi, St. Francis Girls (Mbeya).

Wengine ni Beatrice Issara wa shule ya St. Mary Goreti (Kilimanjaro), Johnston Dedani Ilboru (Arusha) na Samweli Emmanuel wa Moshi Technical (Kilimanjaro), Bertha Sanga, Marian Girls (Pwani) na Bernadetha Kalluvya wa St. Mary Goret (Kilimanjaro).

Washindi hao ni miongoni mwa wasichana 216,084 sawa na asilimia 47.17 waliosajiliwa kufanya mtihani huo mwaka jana. Wavulana walikuwa 242,030 sawa na asilimia 52.83, jumla ya watahiniwa wote walikuwa 458,114.

Jumla ya watahiniwa wa shule 177,021 sawa na asilimia 50.40 ya waliofanya mtihani wa kidato cha nne 2010 wamefaulu , ambapo wasichana waliofaulu ni 69,996 sawa na asilimi 43.47 na wavulana 107,025 sawa na asilimia 56.28.

Idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 46,064 sawa na asilimia 52.09 ya waliofanya mtihani.

Wakati huo huo, NECTA imesitisha kutoa matokeo ya watahiniwa 1,448 waliofanya mtihani bila kulipa ada ya mtihani hadi hapo watakapolipa pamoja na faini katika kipindi cha miaka miwili, tangu tarehe ya matokeo kutangazwa rasmi.

Bi. Ndalichako alisema kuwa baada ya muda huo kumalizika matokeo yao yote yatafutwa kwa mujibu wa kifungu 52 (b) cha kanuni za mitihani.

Pia wanafunzi wenye namba S0358/ na S0243/0007 waliofanya mtihani wa kidato cha nne Oktoba mwaka jana kwa kutumia sifa zinazofanana hawatapatiwa matokeo yao hadi wakuu wa shule watakapowasilisha nyaraka zinazothibitisha uhalali wao.

Pia mwanafunzi mwenye namba S3484/0014 anayetuhumiwa kufanya mtihani kwa kutimia sifa za mtu mwingine, uamuzi kuhusu matokeo yake utatolewa baada ya kukamilika kwa uchunguzi unaofanyika kuhusu uhalali wa sifa zake.

NECTA pia imefuta matokeo na kuwaondoa katika usajili wa mtihani huo watahiniwa wenye namba S1461/0060 na S1461/0146 wa shule ya sekondari Kisaka na S2777/0033 na S2777/0083 wa shule ya sekondari Nguvu Mpya waliofanya mtihani kwa kutumia sifa za watahiniwa wengine.

"Wengine waliofutiwa matokeo na kuondolewa katika usajili ni watahiniwa 35 wa shule ya sekondari Bara, waliosajiliwa katika shule hiyo kwa kutumia majina ya watahiniwa ambao walichaguliwa kujiunga na shule hiyo lakini hawakwenda kuripoti," alisema.

Alimtaja mtahiniwa mwingine aliyefutiwa matokeo kuwa ni wa shule ya sekondari Ludewa aliyefanya mtihani kama mtahiniwa wa shule wakati hakuwa miongoni mwa waliosajili.

Bi Ndalichako alisema watahiniwa wanne wenye namba S 1457/0004, S1457/0006,S1457/0039 na S1457/0027 wa shule ya sekondari Ibanda nao wamefutiwa matokeo kutokana na kutokuwa wanafunzi halali wa shule hiyo.

"Wataniwa wengine 42 wamefutiwa matokeo ni kutoka shule za Ujenzi, Kahama Muslim, John's Seminary, Eckernford, Seuta, Jamhuri, Madanya New Vision na Mseru waliofanya mtihani wakati walikuwa wameondolewa katika usajili baada ya kubainika kuwa sifa za kidato cha pili walizowasilisha hazikuwa sahihi.

Aliwataja watainiwa wengine wanne wenye namba S3526/0066, S0545/0066, S0859/0116, P0328/262 wamefutiwa matokeo baada ya kuandika matusi katika kitabu cha majibu ya Biolojia Geografia, Historia na Kemia.

Bw. Ndalichako alisema NECTA pia imefuta usajili wa kituo cha watahiniwa wa kujitegemea P1189 Biafra Dar es Salaam kutokana na kukiuka taratibu za uendeshaji mtihani.

No comments:

Post a Comment