27 January 2011

Muro alimfunga pingu Wage- Shahidi

Na Rabia Bakari

SHAHIDI katika kesi ya kuomba rushwa ya sh. milioni 10, inayomkabili Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni  ya Taifa  (TBC1), Bw. Jerry Muro na
wenzake, SSP Duwan Nyanda amedai kuwa mshtakiwa huyo alimfunga pingu Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bw. Michael Karoli Wage wakati akimtisha na kumuomba rushwa.

SSP Nyanda ambaye ni shahidi wa sita, alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi, Bw. Gabriel Mirumbe anayesikiliza kesi hiyo.

Alidai Bw. Wage alimueleza kuwa Bw. Muro alitumia  pingu kumfunga wakati anamtishia na kumuomba rushwa.

Katika ushahidi wake, shahidi huyo alidai kuwa mnamo Januari 31,2010, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bw. Charles Mkumbo alimtaka asimamie upekuzi katika gari aina ya Toyota Cresta nyeupe ya Bw.Muro lenye namba za usajili T 545 BEH ili  kuthibitisha kama kweli ndani kulikuwa na vitu vilivyodaiwa na Bw. Wage ambapo pia alidai kusahau miwani katika gari hilo.

“Nilipofanya upekuzi nilipata pea moja ya miwani, ambayo Wage aliitambua kuwa ni ya kwake,  pea moja ya pingu ambayo Wage alidai kuwa ilitumika kumfunga wakati akitishwa na Muro,”alidai SSP Nyanda.

 Alidai kuwa baada ya kupata vitu hivyo aliviandika katika hati ya upekuzi ambayo Bw. Muro aliisaini, yeye mwenyewe pia aliisaini pamoja na askari Lugano.

Baada ya kueleza hayo, Nyanda aliiomba mahakama ipokee hati hiyo ya upekuzi, miwani na pingu kama sehemu ya vielelezo katika kesi hiyo kama upande wa utetezi utakuwa hauna pingamizi.

Mawakili wa utetezi wanaowatetea kina Muro, Bw. Richard Rweyongeza, Bw. Paschal Kamara na Bw. Majura Magafu walidai kuwa hawana pingamizi  na hivyo mahakama ilivipokea kama vielelezo katika kesi hiyo.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu  Mirumbe aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 7 na 8, mwaka 2011 itakapoendelea kusikilizwa tena.

Wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Bw. Deogratius Mgasa na Bw.Edmund Kapama.

3 comments:

  1. Hii kesi ya Jerry Muro ingesambaa mpaka kwa wezi wote wa RICHMOND, DOWANS, NK mbona watanzania tungejenga nidhamu!

    Palipo na Kesi hapafunguliwi, penye mushkeli kesi kila siku! Hebu tuache mahakama itatuambia ukweli!

    Sisi yetu macho na masikio! Lakini sasa ifikie mwisho haya mambo mahakimu muyamalize kila siku mnahairisha kesi. Mwishowe tutadhania "The right delayed is the right denied" Tumechoka kusikia kila siku kesi imehirishwa hadi tarehe.

    Muda wote huu bado ushahidi haujakamilika tu?! Sasa kesi ilifuguliwa ya nini kama hakuna ushahidi au ushahidi una mashaka!

    By Carwin

    ReplyDelete
  2. Tangu nianze kufuatilia sakata la Muro hadi shauri lake limepoanza kusikilizwa nashangazwa na jambo moja kwamba Wage alitishiwa na Muro kuuwawa ili atoe rushwa ya Shs. milioni 10 kwamadai yakutokujumuishwa katika shauri la Lyumba.

    Jambo la msingi lakujiuliza ni je hili tishio lilikua la muda gani? Ni ngumu kuingia katika akili ya mtu anyefikiri sawasawa kwamba madai ya Wage yanamsingi.

    Utaona kwamba, tukio zima limetokea katika kipindi cha zaidi ya siku moja( yaani eti leo Wage anaitwa anatishiwa kisha anarudi kwake halafu siku nyingine anaitwa tena anatishiwa halafu anarudi kwake, n.k). Jambo la kuhoji ni uwepo wa kitisho hicho, maana utaona kwa nafasi yake Wage alikua anaweza kutoa taarifa ya kitisho hicho Polisi, siku ya kwanza tu alipotishiwa na kuachiwa. Lakini yeye hakufanya hivyo. Ni vigumu kuamini mtu aliyetishiwa maisha tena kwa bastola apatapo mwanya wakua huru ashindwe kutoa taarifa polisi mara moja na badala yake kuendelea kutii maelekezo ya mtu aliyekupa kitisho wakati kitisho hicho hakikuendelea kuwepo.Dhana ya kitisho ndiyo huwa iko hivyo. Huwezi ukatishiwa maisha tena kwa bastola na mtu unaemtambua halafu ukakaa kimya. Jamani hivi ni mara ngapi watu mbalimbali hapa nchini kwetu wamekua wakipokea ujumbe wakutishiwa maisha tena kwa ujumbe wa simu( SMS) toka kwa watu wasiowafahamu na bado wakatoa taarifa polisi na hata katika vyombo vya habari?

    Shauri la Muro ni lakuliangalia kwa umakini lisije likaweka mfano mbaya wamatumizi wa mkondo wa sheria katika maslahi ya mtu au kundi fulani. Masuala ya bastola na pingu hayawezi kujustify madai ya wage. Hivyo ni vitu ambavyo Muro anavimiliki kisheria na anaruhusa yakutembea navyo popote. Ama tumesahau ya Ditopile? Suala lakua na bastola halikua mjadala kwani aliimiliki kihalali. Jambo la msingi ilikua matumizi yake. sasa hili la Muro linatia shaka kubwa, maana mtu anaweza kufahamu kuwa unamiliki silaha hiyo na akadai kuwa umeitumia kwa kumtishia.

    Tukumbuke kuwa ni siku chache tu Muro alipata kulalamika kutishiwa maisha. na taarifa zikwa katika vyombo vya habari. Tukumbuke zaidi pia Muro alipambana na jeshi la polisi ktk kufichua rushwa ya matrafiki na askari kadhaa wakapoteza kazi, na pia jeshi zima kupoteza imani kwa wananchi. Sasa mazingira yote haya si yakuyafumbia macho.

    Nionavyo mimi, madai ya Wage yanatia mashaka sana hasa dhana yakutishiwa maisha tena kwa bastola na kwa vipindi tofauti tofauti ambapo alikua na nafasi yakutoa taarifa polisi na polisi wakalifuatilia jambo hilo tangu hatua za awali.

    Maoni yangu ni hayo tu.

    ReplyDelete
  3. Pole sana Muro mpiganaji hii kesi kuna namna!! Hakimu anabidi awe mwaanagalifu ktk suala hili, tokea mwanzo kuna mapungufu mengi, tena inaonyesha ni ya kupangwa pangwa,nadhani pia ni njia ya wage kutaka kupoza makali ya kesi yake ya ubadilifu huko Bwagamoyo!!Mwanzo alidai alionyeshwa pingu na Muro akikaidi amfunge nazo, leo cha ajabu imeshakuwa aliwahi kufungwa hizo pingu, pili iweje mtu kaleta pesa za rushwa apewe Muro kabla hajazipokea au kumkabidhi anawekwa chini ya ulinzi,wao walishajipanga wamkamate na ushahidi iweje wawahi kumbambikia inaingia akilini?

    ReplyDelete