Na Elizabeth Mayemba
WASHINDI wa Tuzo za Kilimanjaro Music Awards wa mwaka jana, wametunga wimbo wa pamoja ambao utaanza kurushwa kwenye vituo vya televisheni na
redio kwa ajili ya kunadi tuzo za mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Meneja wa bia ya Kilimanjaro, Geoege Kavishe alisema tuzo za mwaka huu zimeboreshwa kwa hali ya juu na mchakato wa kupata nyimbo bora unafanywa na watu maalumu ambao wameweka rekodi za kazi zote zilizofanywa na wasanii mwaka jana.
"Mwaka jana tuzo hizi za muziki zilifanyiwa mabadiliko makubwa, ambayo yataendelezwa na kuboreshwa zaidi mwaka huu, mchakato wa kuwapata vinara hao utapitia katika hatua mbalimbali," alisema Kavishe.
Alisema hatua mojawapo ni Academy yenye mkusanyiko wa wadau wa muziki 100 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, ambao huwekwa pamoja katika eneo moja kuwawezesha kuchanganua na hatimaye kupata wateule wa vinyang'anyiro mbalimbali na kwamba utaratibu huo haujabadilika ambao mwaka huu utafanyika Februari 12 na 13 mwaka huu.
Pia majaji watakuwa na kazi moja kubwa ya kuhakiki uteuzi wa wateule uliofanywa na Academy hiyo, ikiwa ni pamoja na kura zitakazopigwa na wananchi na kwamba wao hutumia zaidi vigezo halali vinavyopatikana na mkusanyiko wa rekodi za wasanii zilizotoka kwa mwaka jana.
No comments:
Post a Comment