25 January 2011

Wahitimu ualimu wazua tafrani wizarani

Na Benjamin Masese

SAKATA la baadhi ya walimu waliohitimu mwaka 2009/2010 la kuvamia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi kudai ajira limeingia sura mpya baada ya
jana kuzua tafrani kati yao na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Hamisi Dilenga wakati akiwaeleza utaratibu uliopangwa na Utumishi kuajiri.

Bw. Dihenga aliwaeleza kwamba Wizara ya Utumishi ndio yenye mamlaka ya kutoa nafasi za ajira na hivi sasa imesitisha rasmi mpango uliokuwepo wa kuwapa ajira walimu waliofeli baadhi ya masomo yao na kuwapa muda wa miaka miwili kuyarudia.

Alisema kuwa baada mpango huo kusitishwa ghafla wizara ya elimu ililazimika kufanya mazungumzo na baadhi ya vitengo vinavyohusika, ambapo walikubaliana kwamba walimu hao wanatakiwa kusajiliwa upya katika vyuo ili kurudia masomo hayo kabla ya Mei mwaka huu ili wapeww ajira, kitendo kilichozua zomeazomea na maswali mengi.

Maneno makali ya kukaripiana kati ya walimu na Bw. Dihenga yalitawala wizarani hapo, hali iliyomfanya kiongozi huyo kuwahoji kama wanatambua wanayeongea naye na ana nafasi gani kwao, ndipo walizidi kumhakikishia kwamba wanachohitaji ni haki yao na sio kuangalia cheo chake.

Ilifikia wakati Bw. Dihenga kutoa majibu ya mkato na kwa hasira kulingana na maswali yaliyokuwa akiulizwa kwamba kuna walimu waliofeli na wameajiriwa na wengine ambao hawakufeli wameachwa.

Bw. Dihenga alisema kwamba wizara ya elimu haina mpango wowote wa kutoa ajira nyingine kulingana na maagizo kutoka wizara ya utumishi na kuongeza kwamba cha kuwasaidia ni kuwaombea Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) kupokea fedha zao za usajili ili kurudia mtihani wa masomo waliofeli.

Walimu hao walisema kwamba hawako yatari kurudia mtihani huo kwa madai kwamba wizara imetoa ajira ya kujuana kwani kuna walimu walifeli zaidi ya masomo matatu, wanafahamu kwa majina lakini wameajiriwa huku.

Bw. Dihenga alitoa tamko kwamba walimu wote walioajiriwa huku wakiwa hawakufaulu masomo yao watanyang'anywa ajira hiyo na kuwapa waliofaulu hata kama walisharipoti shuleni.

Baada ya maswali kuzidi, Bw. Dihenga alivunja kikao kwa hasira na kusema tafuteni mwingine anayeweza, pia nendeni mnapoweza, lakini mtarudi kwangu, hali iliyosababisha walimu kwenda Ofisi za Waziri Mkuu na kukumbana na askari wa kutuliza ghasia getini na kuwaziua kuingia.

Askari hao ambao tayari walikuwa wamejiandaa kwa lolote, waliwataka kuondoka hapo haraka kwa sababu sio sehemu ya kufanya mikusanyiko, pia waliwataka kuandika barua ya kumuona Bw. Pinda kwa siku maalumu.

Awali, walimu hao walianza kumzuia Waziri wa elimu Dkt. Shukuru Kawamba asiondoke ofisi hapo hali iliyosababisha ulinzi kuimarishwa ambapo waliamua kubandika mabango kwenye majengo ya wizara hiyo.

Baadhi ya mabango yalisomeka kwamba "Nini kazi ya Kawambwa, ni kukimbia majukumu yako au kufumbia macho kilio chetu, JK timiza ahadi zako za ajira kwa walimu au fedha ndizo mnazotaka kulipa Dowans, tumechoka na ubabaishaji wa serikali hii jamani adhabu yake ni mwaka 2015 tufanye kweli.  

2 comments:

  1. duh mazito sana! hayo maneno ukiyapima dhahiri yanataka uyaelewe hawakusudii hakuna kazi wala hawawezi kusaidia ila kinachotakiwa ni maelewano ya kiswahili yaani baina ya viongozi na muomba kazi{uengeze uzito}ili file lako lishuke chini ya desk.

    ReplyDelete
  2. Ni ajabu sana ! mbona kuna wengi wamefeli siku za nyuma na wanadunda mzigo kama hawana akili nzuri? Pengine hao waliofeli wanaweza kufanya kazi nzuri kuliko waliofaulu. Mbona mitihani si kipimo cha utendaji tena? Tutafute kipimo cha maadili kwanza. Ona sasa wanamtukana mtu anayeatakiwa kuwaajiri.

    ReplyDelete