Na Elizabeth Mayemba
UONGOZI wa klabu ya Simba umewapa wachezaji wake sh. milioni 15 ikiwa ni zawadi baada ya kufanikiwa kuchukua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.Simba juzi ilifanikiwa kuwafunga mahasimu wao Yanga mabao 2-0, katika
mchezo wa fainali wa michuano hiyo uliochezwa Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu ya Simba, Cliford Ndimbo alisema sh. milioni 10 zilitolewa na uongozi kama zawadi kwa wachezaji wake na sh. milioni tano ni zawadi ya mshindi wa kwanza.
"Tumetoa kiasi hicho cha fedha kama motisha kwa wachezaji wetu, baada ya kufanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi na hiyo ni changamoto kwao, ili mashindano yanayokuja wafanye vizuri zaidi," alisema Ndimbo.
Alisema timu hiyo imeleta heshima kubwa mbele ya mashabiki wao ikiwa na kuwafunga mahasimu wao wakubwa Yanga, ambao mara ya mwisho walipocheza nao walifungwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa kwanza.
Ndimbo alisema timu hiyo, inatarajiwa kuwasili Dar es Salaam kesho. Wachezaji hao walikuwa katika mapumziko kwa sababu mechi hiyo ilichezwa usiku, hivyo wakaona ni vyema wakapewa mapumzika kwanza.
Alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri ataendelea na programu yake ya mazoezi kwa ajili ya kuwaandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment