Na Emmanuel Msigwa, Songea
MKAZI wa Kota za Majengo katika Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, Bi. Juliana Ngimba , amejikuta katika wakati mgumu yeye pamoja na familia yake baada ya nyumba aliyokuwa amepanga kubomolewa paa ikiwa ni
shinikizo la kumtaka ahame katika nyumba hiyo.
Amri hiyo imekuja baada ya halmashauri ya Manispaa ya Songea ambayo ilikuwa ikiimiliki nyumba hiyo, kukiuzia Chama cha Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Manispaa hiyo kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Majira ilishiuhudia nyumba hiyo ikiezuliwa paa Januari 12 mwaka huu saa 3 asubuhi bila mhusika anayeishi katika nyumba hiyo kuwepo.
Akizungumza na Majira katika eneo la tukio Makamu Mwenyekiti wa SACCOS hiyo , Bw. Athuman Luambano alisema Bi. Juliana aliamriwa na mahakama ya Nyumba na ardhi wilayani Songea tangu Oktoba 26 mwaka jana. ili kupisha ujenzi wa ukumbi wa chama hicho.
“Hukumu ya kumtaka mpangaji huyu kuondoka ilitolewa tangu mwezi wa kumi mwaka jana lakini akawa mbishi kuondoka hadi tulipoamua kukabidhi jukumu hili kwa Dalali Nyamaka Action Mart ambapo walifanya mazungumzo na akaahidi kukabidhi funguo Januari 8 mwaka huu lakini hakufanya hivyo,” alisema Bw. Luambano.
Alisema hatua ya kuezua paa la nyumba hiyo ilihali ndani kukiwa na mali za mwanamke huyo haziwahusu kwakuwa madai kuwa hiyo ni hatua ya awali kuezua bati nyumba hiyo na kisha kuibomoa tayari kwa kuanza kuchimba msingi kwa ajili ya kujenga ukumbi wa chama chao.
Naye Bi. Juliana alisema hivi sasa hana kwa kwenda na ataendelea kuishi katika nyumba hiyo hata kama imeezuliwa paa licha ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha huku akidai kuwa ameishi katika nyumba hiyo tangu mwaka 1982 ikiwa mikononi mwa Shirika la Nyumba la Taifa.
Juhudi za gazeti hili kumpata Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Bw. Naftary Saiyoloi kuzungumzia sakata hilo ziligonga mwamba baada ya kuambiwa yupo safarini Dodoma kikazi.
No comments:
Post a Comment