26 January 2011

TFF 'yaichakachua' Kamati ya Waamuzi

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeifanyia mabadiliko Kamati ya Waamuzi kwa kumuondoa aliyekuwa Mwenyekiti, Shaibu Nampunde na
kumteua Kapteni Mstaafu, Stanley Lugenge kuwa Mwenyekiti ili kuongeza ufanisi katika kamati hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo iliyokutana Januari 16, mwaka huu imepitisha majina ya wajumbe waliopendekezwa kuunda kamati ndogo ndogo za shirikisho hilo.

Alisema kamati hizo zitakaa madarakani kwa miaka miwili na kufanya kazi kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ambapo miongoni mwa kamati hizo, Kamati ya Waamuzi ndiyo iliyofanyiwa mabadiliko makubwa.

"Mabadiliko hayo makubwa ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti, Nampunde sasa ataongoza Kamati ya Ufundi na Maendeleo ambapo Kapteni Mstaafu Lugenge atachukua nafasi yake akiwa na Wajumbe, Omari Kasinde, Riziki Majalla, Joan Minja na Mohamed Nyama," alisema Wambura.

Alisema wajumbe Llody Nchunga na Jamal Bayser, wamehamishiwa kamati nyingine kutoka ile ya Nidhamu kutokana na mgongano wa kimaslahi ambapo sasa Bayser anakuwa Mjumbe wa Kamati ya Habari na Masoko na Nchunga yupo kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za wachezaji.

Wambura pia alizungumzia mchezo wa kirafiki kati ya timu ya taifa 'Taifa Stars' na Palestina utakaopigwa Februari 9, mwaka huu kwamba maandalizi yanaendelea vizuri.

Alisema licha ya kuwepo kwa mchezo huo, TFF itahakikisha kabla ya kuumana na Afrika ya Kati Machi 26, mwaka huu inaipatia mchezo mwingine wa kujipima nguvu timu hiyo ili ifanye maandalizi ya uhakika

No comments:

Post a Comment