26 January 2011

Yanga, TFF zapishana kauli

*Ni kuhusu mechi na Dedebit
*Papic atangaza kujiuzulu


Na Elizabeth Mayemba

WAKATI uongozi wa Yanga, ukitangaza mechi yao dhidi ya
Wahabeshi, Dedebit FC itapigwa Uwanja wa Taifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) nalo limetangaza kuwa mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo kauli mbili tofauti kati ya Yanga na TFF, inaonekana kuwakoroga viongozi hao wa pande mbili kuhusiana na mechi ya michuano ya Shirikisho.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Michael Wambura alisema kuwa shirikisho hilo liliwasiliana na viongozi wa Yanga kwamba mechi hiyo itachezwa Jumamosi katika Uwanja Uhuru, Dar es Salaam.

Huku TFF itangaza hivyo, Yanga nayo kupitia Ofisa Habari wake Louis Sendeu, alisema jana kuwa mchezo huo utapigwa Uwanja wa Taifa na pia alitangaza viingilio cha mechi hiyo.

Sendeu alisema VIP A wataingia kwa sh. 20,000, VIP B sh. 10,000, VIP C sh. 5,000 na viti vilivyobakia ni sh. 3,000.

"Tumeamua kuweka kiingilio cha chini kabisa ili kuwawezesha mashabiki wa soka nchini waweze kuhudhuria katika mchezo wetu, ili kuishangilia timu yetu inayoiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa," alisema Sendeu.

Alisema wapinzani wao wanatarajia kutua nchini kesho, pamoja na waamuzi wote watakaochezesha mchezo huo, ambao wanatoka Sudan na kamisaa anatokea Namibia.

Sendeu alisema wanatarajia mashabiki wote nchini wataungana kwa ajili ya kuishangilia timu yao kwa nguvu ili ipate ushindi.

Alisema timu yake inaendelea na mazoezi kama kawaida katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na lengo ni kushinda mchezo huo ili waweze kusonga mbele katika michuano hiyo.

Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic jana ametangaza kujiondoa katika klabu hiyo.

Sendeu alisema kuwa kocha huyo inadaiwa ameamua kuchukua uamuzi huo, baada ya kutangazwa Felix Minziro kuwa msaidizi wake ambaye yeye hakuta awe yeye.

1 comment:

  1. huyu Papic ni mtu wa ajabu.sasa anakataa kuwa na kocha msaidizi mwenye uwezo wa kufundisha wakati aliomba kazi ya kufundisha timu yetu ya taifa, je angetuchagulia kocha ambaye hana uwezo kumsaidia kufundisha timu yetu ya Taifa? yaani kocha ambaye tunamwamini ana uwezo mkubwa wa kufundisha anamuogopa Minziro? hii ni aibu sana kwake.mi nafikiri akipata msaidizi mwenye uwezo inampungizia majukumu na kazi zinaenda vizuri hata kama yeye hayupo kwa dharura timu bado itakuwa katika kiwango kizuri. viongozi wa Yanga achaneni na huyo Papic mpeni chake tafuteni kocha mwingine. yeye ni mwajiriwa wa yanga na minziro ni mwajiriwa vile vile inakuwaje tena aanze tuchagua mtu wa kufanya naye kazi? aende zake Yanga aliikuta na ataiacha kama ilivyo.

    ReplyDelete