26 January 2011

Tanzania, Cuba kusaidiana tiba ya malaria

Na Dunstan Bahai

SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na ile ya Cuba, zinakusudia kujenga kiwanda cha kuzalisha viatilifu vya kupambana na vimelea vya malaria.Uamuzi huo
wa serikali ulitangazwa jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hadji Hussein Mponda wakati akifungua Warsha ya siku moja ya Mradi wa Upatikanaji wa Dawa Mseto za bei nafuu kwa sekta binafsi iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema kwamba kiwanda hicho kinachotarajiwa kujengwa mjini Kibaha mkoani Pwani, kitazalisha viatilifu ambavyo vitatumika kunyunyiza katika mazalia ya mbu ili kuua viluwiluwi vya mbu.

Viatilifu hivi si kemilikali na havitaathiri mimea wala wanyama, alisema na kuongeza kuwa ni rafiki wa mazingira na vitakuwepo kwa ajili ya kupambana na mazalia ya mbu tu.

Kwa mujibu wa waziri huyo, kiwanda hicho kitakuwa pekee katika nchi za Afrika Mashariki na kwamba mbali na masuala ya afya, yaani kupambana na mbu, pia kiuchumi kitaliingizia taifa fedha nyingi baada ya kuviuza viatilifu hivyo katika nchi jirani kama za Kenya na Uganda.

Akizungumzia athari za ugonjwa wa malaria ambao alisema ndio unaoongoza kwa vifo duniani na hasa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, alisema takwimu zinaonesha kuna matukio kati ya milioni 10 na 12 ya malaria kila mwaka nchini, na kwamba ugonjwa huo unaongoza kwa mahudhurio ya wagonjwa wa nje hospitalini, ikiwa ni sawa na asilimia kati ya 30 na 40 ya magonjwa yote.

Inakadiriwa kwamba kuna vifo kati ya 60,000 na 80,000 kila mwaka vinavyotokana na malaria na  asilimia 80 ya vifo hivyo hutokea nyumbani na havitolewi taarifa. Waathirika wakubwa wakiwa ni watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano na mama wajawazito, alisema.

Mbali na matukio hayo ambayo yanawakumba watu, katika suala la uchumi Tanzania na nchi nyingine zinaingia hasara kubwa ambapo kwa Tanzania peke yake inapoteza asilimia 3.4 ya pato lake kutokana na ugonjwa huo.

Hata hivyo, alisema serikali imekuwa ikifanya kila jitihada katika kutokomeza ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kusambaza vyandarua vyenye dawa, upulizaji dawa ukoko majumbani, udhibiti wa mazalia ya mbu na matumizi ya dawa ya SP kwa mama wajawazito lakini pia na matumizi ya dawa mseto.

Kuhusu vyandarua, alisema tayari tangu kampeni hizo zianze, vyandarua 8,750,000 vimeshasambazwa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano na vinaendelea kutolewa bure kwa kila kaya na kwamba hadi kazi hiyo itakapokamilika Mei mwaka huu, zaidi ya vyandarua milioni 15 vinatarajiwa kutolewa.

1 comment:

  1. JAMANI MBONA SIJASIKIA WAWEKEZAJI WA MIRADI YA KUTHIBITI UFISADI?? HATA MKITHIBITI HAYO MALARIA LAKINI HUYO MWANACHI FEDHA ZAKE ZINAPORWA NA MAFISADI SI BORA AFE KWA MALARI AKULIKO KUFA KWA KUKOSA FEDHA ZA KUJIKIMU??

    ReplyDelete