26 January 2011

Mtego wa jerry Muro wawekwa bayana

Na Rabia Bakari

SHAHIDI wa nne katika kesi ya kuomba rushwa ya sh. milioni 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa kituo cha televisheni cha TBC1, Bw. Jerry Muro na
wenzake, Inspekta Msaidizi wa Polisi Issa Seleman (37) ameieleza mahakama jinsi alivyoweka mtego na kufanikiwa kumkamata Bw. Muro.

Inspekta Seleman alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wakati kusikilizwa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi, Bw. Gabriel Mirumbe anayesikiliza kesi hiyo.

Akiendelea kutoa ushahidi wake huku akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Bw. Boniface Stanslaus alidai mnamo Januari 30,2010, majira ya saa 4:00 asubuhi, akiwa kwenye kazi za nje alipokea simu kutoka kwa Sajenti Gervas ikimtaarifu kuwa kuna watu wamemtishia na kumuomba rushwa ya sh. milioni 10, Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage.

"Baada ya kupata taarifa hizo, nilikwenda ofisini na kumkuta Sajenti Gervas akiwa na Wage ambaye alinieleza malalamiko yake ya kutishiwa na kuombwa rushwa ya sh. milioni 10 na Muro," alidai shahidi huyo.

Aliongeza kudai kuwa baada ya kuyasikiliza malalamiko hayo, aliwasiliana na viongozi wake akiwepo Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Ilala, SSP Duwan Nyanda ambaye alimuamuru kufungua jalada la uchunguzi na utaratibu wa kuwakamata Bw. Muro na wenzake ufuatwe.

Baada ya kupata maelezo hayo, Inspekta Seleman alidai kuwa walifungua jalada la uchunguzi na kumtaka Bw. Wage awasiliane na watu waliomtisha na kumuomba rushwa mbele yao.

Alidai wakati wanawasiliana na Bw. Muro, Bw. Wage  alimtaka wakutane katika geti la TBC lakini akakataa na kumtaka wakutane Bamaga.

"Lakini nilimwambia Wage ampigie Muro amwambie kuwa wakutane kesho yake yaani Januari 31, 2010 saa 4 asubuhi katika Goteli ya City Garden.

 "Siku hiyo ilipofika mimi kama Inspekta wa zamu, niliamuru Sajenti Omar na Koplo Masaka wakae nje ya hoteli na mimi na Sajenti Gervas tubakie ndani ya hoteli hiyo," aliongeza kudai.

Alidai kuwa nyakati za saa 6 mchana, Muro aliwasili hotelini hapo na kumtaka Wage atoke nje ya hoteli hiyo ili waonane na kwamba iliwabidi wao wajipange kwa kutumia ishara.

Wage alibeba sweetcase kutaka kuingia ndani ya gari la Muro lakini kabla hajaingia nilimuamuru ashuke na nikamuuliza Muro kama anamfahamu Wage, yeye akajibu kuwa hamjui ila Wage yeye alisema anamfahamu Muro na ni mmoja kati ya watu waliokuwa wakimtisha na kumuomba rushwa, alidai Inpekta Seleman.

Aidha katika ushahidi wake alikiri kuwa hakuwahi  kumuhoji Bw. Muro wala kumpekua katika gari yake.

Shahidi wa tano katika kesi hiyo, Inspekta Anthony Mwita (45) alidai mahakamani hapo kuwa Februari 2, 2010  alikwenda katika Hoteli ya Sea Cliff kuonana na Meneja wa Kitengo cha IT ili awapatie picha za kamera za CCTV   za watu waliongia na kutoka Januari 29, 2010.

Pamoja na kuangalia picha za CCTV, pia alidai kukagua kitabu cha kumbukumbu ya wageni na kilikuwa na  kumbukumbu ya usajili wa gari la Muro lenye namba za usajili T 545 DEH aina ya Cresta ambalo lilipewa kadi namba 673 ya hoteli hiyo ya Sea Cliff ambalo liliingia saa 7:33 mchana na kutoka saa 8:48 mchana.

Pia katika ushahidi wake, alidai kuwahi kukabidhiwa stakabadhi ya kununulia pingu yenye namba 34357310 aliyoinunua kwa sh 25,000 katika duka la jeshi la Mzinga lililopo Upanga Mei 26, 2009, ambapo pia baada ya kufanya upelelezi katika duka hilo, walinithibitisha kuwa ni kweli duka hilo lilimuuzia pingu.
 
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Bw. Deogratius Mgasa na Bw. Edmund Kapama ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya kuomba rushwa, na kujivika vyeo bandia.Kesho hiyo inaendelea leo kwa mashahidi upande wa mashtaka kuendelea kutoa ushahidi wao.

3 comments:

  1. si mnaona wanavyojichanganya wenyewe

    ReplyDelete
  2. Mie sijaelewa mbona huo ushahidi wa kukutwa anatoa rushwa sijausikia? kama hawana jipya kesi ifungwe

    ReplyDelete
  3. Hata mimi nilitegemea huyo shahidi aseme kuwa alimnukuu Bwana Muro akiomba au kupokea hiyo rushwa. Pili nilitegemmea hiyo pingu ya Muro labda iwe ni moja cha vielelezo vya kutishia malipo ya rushwa. Hiyo ni kesi ya kupanga, Said mwema hana jipya na vijana wake.

    ReplyDelete