Na Wilhelm Mulinda, Mwanza
UJENZI wa Barabara ya Geita-Usagara mkoani Mwanza kwa kiwango cha lami unatarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi sita kuanzia sasa, imefahamika.Akizungumza na
waandishi wa habari jana kwenye eneo la ujenzi huo, Mhandisi Mshauri wa kazi hiyo kutoka Kampuni ya Nicholas O'dwyer kutoka nchini Ireland, Dkt. Giorgio Nicolussi alisema kuwa kwa sasa kazi zilizobaki ni kupaka rangi na kuweka alama barabarani.
Dkt. Nicolussi alisema kuwa kazi zingine zilizobaki ni pamoja na kujenga mitalo, kukamilisha ujenzi wa nyumba tano za wafanyakazi wa mizani, jengo la ofisi na uzio wa magari yanayosubiri kulipa faini pamoja na kufunga mzani magari katika eneo la Usagara.
Alisema kuwa barabara hiyo ambayo ilianza kujengwa mwaka 2008 ilitakiwa kukamilika mwaka 2010, lakini imechelewa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuchelewa kuanza kazi kwa Mkandarasi wa Barabara hiyo, Kampuni ya Sino Hydro Corporation kutoka China.
Kwa mujibu wa Dkt. Nicolussi, sababu zingine ni kuchelewa kulipwa kwa mkandarasi pamoja na mkandarasi kuwa na wafanyakazi wachache ilikinganishwa na ukubwa wa kazi.
"Kwa maana hiyo ili mambo yaende vizuri mkandarasi anatakiwa kukamilisha kazi yake ndani ya miezi mitatu aliyoongezewa na serikali ndipo barabara hiyo iweze kukamilika ndani ya miezi sita kwa vile pia kuna kazi zingine ndogondogo ambazo zinaenda pamoja
na ujenzi wa barabara," alisema.
Hata hivyo, mhandisi mshauri huyo alisema kuwa endapo mkanadarasi atashindwa kukamilisha kazi kwa kipindi cha miezi mitatu aliyoongezewa na serikali basi kampuni hiyo ya ushauri itampiga faini kama adhabu kutokana na kuchelewesha kazi.
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TanRoads) mkoani Mwanza, Mhandisi Leonard Kadashi alisema kuwa Barabara ya Geita-Usagara yenye urefu wa kilometa 95 hadi kukamilika utagharimu sh. bilioni 79.
No comments:
Post a Comment