20 January 2011

Tamasha la Wanyambo laiva Dar

Na Nayla Abdulla

KAMATI ya Maandalizi ya Tamasha la Utamaduni la kabila la Wanyambo wanatarajia kukutana leo katika Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam kwa ajili ya kupanga taratibu za maandalizi ya tamasha hilo.Tamasha hilo la
Wanyambo linatarajia kuanza Januari kuanzia kesho hadi Januari 23, mwaka huu.

Awali tamasha hilo lilipangwa kufanyika Novemba, mwaka jana lakini liliahirishwa kutokana na shughuli za Uchaguzi Mkuu wa nchi uliofanyika Oktoba 31.

Akizungumza Dar es Salaam jana Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Daniel Rutasyamka alisema tamasha hilo litakuwa ni la siku tatu na litahusisha wasanii mbalimbali kutoka Wilaya za Karagwe na Kyerwa pamoja na wadau wengine.

Alisema mambo yatakayofanywa katika tamasha hilo ni maonesho ya ngoma za Wanyambo, Vyakula vya asili, vinywaji vya asili, zana za asili, mila na desturi, nyumba za asili, kazi za mikono, maandishi ya methali, warsha na kongamano zinazozungumzia  maendeleo  ya Karangwe na Kyerwa pamoja na vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika wilaya ya Karagwe na kyerwa.

"Ili tamasha hili liweze kufanikiwa, juhudi za Wanyambo wote waishio Dar es Salaam zinahitajika, hivyo ni muhimu wanyambo wote wa Dar es Salaam kuhudhuria kikao cha kesho (leo)cha maandalizi kitakachofanyika katika kijiji cha makumbusho,"alisema Rutasyamka.

Alisema tamasha hilo litafanyika jijini Dar esSalaam  kwa mara ya kwanza na linategemewa kuwa kiungo  muhimu kati ya Wanyambo waishi Dar es Salaam na Wilaya za Karagwe na Kyerwa.

No comments:

Post a Comment