20 January 2011

Jamhuri yajiweka kando sakata la ZFA

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

KLABU ya soka ya Jamhuri FC ya Pemba imesema, kwamba haihusiki na mvutano wowote unaoendelea, kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).Kauli hiyo ya Jamhuri, imekuja baada ya
klabu hiyo kuhusishwa katika klabu tatu ambazo zimedai kulifikisha mahakamani suala hilo, zikiwemo Zanzibar Ocean View na Miembeni pamoja na taasisi nyengine za soka.

Akizungumzia sakata hilo juzi Katibu Mwenezi wa timu hiyo, Kombo Omar Abdallah alisema timu yake haijashirikiana na mtu yeyote kukaa na kupanga kwenda mahakamani.

“Sisi tusihushishwe na mvutano wowote uliopo huko, hatujashirikiana na mtu wala kupanga kwenda mahakamani, sisi kama uongozi wa timu tutakaa kikao kulijadili hili”, alisema.

"Sisi hivi sasa tunajipanga kwa ajili ya ligi na si vinginevyo," aliongeza katibu huyo.Awali timu hizo zilimwagiza wakili wao kutoka Kampuni ya AJM ‘Solicitors& Advocate Chamber, kuzitaka  mamlaka tatu za michezo kutoa maelezo ya kina juu ya sababu za kushindwa kutekeleza na kusimamia vizuri majukumu yao.

Taasisi zilizotajwa kushindwa kutekeleza majukumu na timu hizo ni Baraza la Michezo la Taifa Zanzibar (BTMZ), Ofisi ya Mrajisi wa Vyama na Klabu za Michezo na ZFA.Timu hizo zilidai kwamba taasisi hizo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kulisababisha ZFA kuendesha kikao batili cha Uchaguzi Mkuu Desemba 31, mwaka jana.

No comments:

Post a Comment