Na Elizabeth Mayemba
UTEUZI wa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu kuwa mdhamini wa Yanga limeonekana kuendelea kuwaumiza vichwa wanachama wa klabu hiyo, ambao wanashinikiza ufanyike Mkutano Mkuu wa dharura ili wajue
mbivu na mbichi.
Wanachama hao wanapinga uteuzi wa Mbunge huyo kwa madai kwamba ana asili ya Simba na pia hajawahi kujitokeza hata siku moja kuisaidia timu kwa namna yoyote walau maji ya kunywa kwa wachezaji.
Pia wanachama hao wanautaka mkutano huo wa dharura kwa kuwa mambo ndani ya Yanga kwa sasa yanakwenda ndivyo sivyo, likiwemo suala la klabu hiyo kuwa kampuni huku viongozi wakiwa hawana umoja.
Hivi karibuni mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, Yusuf Manji alimpendekeza Mtemvu kuwa mmoja wa wajumbe wa bodi ya udhamini, hali ambayo imepingwa vikali na baadhi ya wanachama.
Wakizungumza Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti wanachama hao walidai kwamba wanaona mambo hayaendi sawa ndani ya klabu hiyo na kuna maamuzi yanayofanyika, lakini baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji hawafahamu lolote.
"Ukikaa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ukiwauliza kuhusiana na suala zima la uteuzi wa Mtemvu au Yanga kuwa kampuni, hawafahamu lolote sasa tunataka kuelezwa haya maamuzi yamepitishwa na viongozi wangapi,? alihoji mmoja wa wanachama hao ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini.
Alisema inaonekana wazi kwamba kuna baadhi ya viongozi wa klabu hiyo, hawana msimamo katika maamuzi yao na inaonekana wamekuwa wakiamrishwa kila kitu na mtu mmoja, hali ambayo inazua hofu ndani ya Yanga.
Mwanachama mwingine ambaye hakutaka kuandikwa jina, alisema endapo viongozi hawatakuwa na msimamo wana hofu klabu yao itaelekea kubaya na kwamba wanasikia klabu hiyo inataka kuwa kampuni ili hali wanachama hawajajulishwa lolote.
"Sasa hivi klabu hii inaelekea kubaya sisi kama wanachama tumechoshwa na hali hii na sasa hivi hatutakubali kuendeshwa na mtu yeyote, maana tunaona kama ni utumwa," alisema mwanachama huyo.Hata hivyo kuna taarifa kwamba baadhi ya wazee wa klabu hiyo, jana na juzi walikuwa na kikao na Manji kujaribu kuweka mambo sawa.
No comments:
Post a Comment