24 January 2011

Tamasha la Pasaka kushirikisha nchi sita

Na Mwandishi Wetu

TAMASHA la Pasaka linalofanyika kila mwaka, mwaka huu litawashirikisha wasanii kutoka nchi sita kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam Apili 24, mwaka
huu.

Tamasha hilo kubwa la nyimbo za injili za kumsifu Mungu,  litafanyika wakati wa sikukuu ya Pasaka Aprili 24, mwaka huu, litaandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya jijini Dar es Salaam.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema mwaka huu, litakuwa na tofauti kubwa na matamasha  ya miaka ya nyuma.

"Tumefanya mambo mengi mazuri kuliko ya miaka ya nyuma, waimbaji watakuwa wengi wakiwemo wa kutoka mataifa mengine matano," alisema.

Msama alisema tamasha la mwaka huu limekuwa na maboresha makubwa kwa ajili ya kukidhi matakwa ya wapenzi wa muziki wa injili.

"Tutakuwa na waimbiaji kutoka nchini Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)," alisema.

Lengo la kuwajumuisha wasanii hao ni kutaka kulifanya tamasha hilo kuwa tofauti na miaka mingine.

Msama alisema baada ya tamasha hilo kufanyika jijini Dar es Salaam, watalipeka mkoani Shinyanga Aprili 25 na Mwanza litafanyika Aprili 26, wakati wa sikukuu ya Muungano.

Alisema tamasha hilo litakuwa na kiingilio cha chini zaidi, ili kila mmoja aweze kuhudhuria na kupata baraka kutoka kwa waimbaji hao wanaomsifu Mungu.

"Waimbaji wote maafuru wa muziki wa injili watakuwepo, tumejipanga vizuri kuhakiksha tamasha hili linakuwa gumzo kila mahali," alisema.

No comments:

Post a Comment