24 January 2011

Barcelona yazidi kupaa ligi ya Hispania

BARCELONA, Hispania

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Hispania, Barcelona imeshinda mechi yake ya 14 mfululizo kwenye michuano hiyo, baada ya kuibuka na ushindi wa
mabao 3-0 dhidi ya timu ya Racing Santander.

Wachezaji Pedro Rodriguez na Lionel Messi, ndiyo waliyoipatia mabao timu hiyo kipindi cha kwanza na Andres Iniesta, akaongeza la tatu kipindi cha pili lililoihakikishia timu hiyo kuongeza pengo la pointi saba kwa mahasimu wao Real Madrid, ambao nao jana walikuwa wakiumana na Mallorca.

Katika mchezi huo wa juzi kikosi hicho kinachonolewa na kocha, Pep Guardiola kilitandaza kandanda safi lililokifanya kuweka rekodi ya kufikisha pointi 52 katikati mwa msimu.

Awali Racing iliionekana kama ingeweza kuhimili mikikimikiki ya Barcelona, lakini mchezo wa vinara hao wa Catalan uliohusisha mashuti, pasi za harakaharaka na kasi ndivyo vilionekana kuwalemea wageni hao.

Mchezaji Rodriguez ndiye aliyekuwa wa kwanza kuipatia timu yake bao la kuongoza dakika ya pili ya mchezo, baada ya kutuliza kifuani pasi aliyotengewa na Messi, baada ya nyota huyo wa Argentina kwa kushirikiana vyema na David Villa, kupenya ngome ya wapinzani wao upande wa kushoto na kisha kuachia krosi iliyokutana na mfungaji huyo.

Messi aliyafanya matokeo kuwa 2-0 kwa mkwaju wa penalti dakika ya 33 baada ya Villa, kufanyiwa madhambi akiwa ndani ya eneo la hatari na beki wa Racing, Henrique na Iniesta akaachia mkwaju baada ya kupokea pasi kutoka  Rodriguez na kisha kuwapita kirahisi mabeki kabla ya kuukwamisha mpira huo kimiani dakika ya 56.

Kwa ushindi huo Barcelona, imefikisha rekodi ambayo iliiweka katika michuano ya ligi msimu wa mwaka 2005-06 na bado inahitaji ushindi wa mechi moja kufikisha rekodi ambayo iliwahi kuwekwa na Real Madrid, katika msimu wa mwaka 1960-61.

“Hakuna mechi rahisi,” alisema  Villa. “Lakini tulifanikiwa kuongoza dakika ya pili na ndiyo maana presha ikatushuka. Kwa sasa tunachoangalia ni kama tutakuwa na bahati kwa kesho (jana) kama Real Madrid hawatashinda,” aliongeza.

No comments:

Post a Comment