*Baada ya Azam kuifunga Simba 3-2
Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, timu ya Simba, jana ilianza vibaya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu baada ya kuchapwa mabao 3-2 na
Azam FC, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati mchezo ukiendelea, kipa wa Simba, Juma Kaseja alilia na kuomba kutoka nje kutokana na kufungwa bao la tatu na John Bocco 'Adebayor' dakika ya 54.
Nahodha wa Simba kwa jana, Mussa Hassan 'Mgosi' pamoja na wachezaji wengine ilibidi wafanye kazi ya ziada kumuomba aendelee na mchezo ambapo alifanya hivyo, huku akiendelea kulia na baadaye aliamua kunyamaza.
Katika mchezo huo wa jana, timu zote zilianza soka la kupooza lakini dakika ya tano, Azam ilifanya shambulizi la ghafla kupitia kwa Jamal Mnyate aliyeunasa mpira uliopigwa vibaya na beki, Haruna Shamte na kupiga shuti lililotoka nje.
Simba ilitulia na kufanya shambulizi la nguvu dakika tatu baadaye, ambalo lilizaa matunda kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Nicco Nyagawa kupiga shuti nje ya eneo la hatari na Mgosi kuugonga na kujaa wavuni huku akimuacha kipa, Vladmir Niyonkuru asijue la kufanya.
Bocco ambaye katika mchezo huo alionekana kung'ara aliisawazishia timu yake bao dakika ya 14 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Mnyate na kabla Simba haijatulia, Mrisho Ngassa alifunga bao la pili dakika ya 23 baada ya kumpiga chenga, Kaseja na kupiga shuti lililojaa wavuni.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo kila timu ilifanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa mpinzani wake ambapo dakika ya 50, Ali Ahmed 'Shiboli' aliyeingia badala ya Nyagawa alipiga shuti lililopanguliwa na Niyonkuru na kuwa kona tasa.
Dakika nne, Azam walifanya shambulizi la kushtukiza ambapo Patrick Mafisango alipiga mpira mrefu uliotua kwa Bocco ambaye aliupiga na kujaa wavuni.
Bao hilo ndiyo lililomtia uchungu Kaseja, ambaye baada ya kufungwa alilia huku akiomba kutoka nje.
Zikiwa zimebaki dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho kipyenga kupulizwa, Hilary Echessa aliifungia Simba bao la pili akimalizia pasi ya Mgosi.
No comments:
Post a Comment