Na Zahoro Mlanzi
KIKOSI cha wachezaji 21 wa timu ya Taifa 'Taifa Stars', kimeondoka jana alfajiri kwenda Misri huku kikiwa na matumaini ya kufanya vizuri katika mashindano ya
Mto Nile.
Timu hiyo itapumzika leo na kesho usiku, itaanza kutupa karata yake kwa kuumana na wenyeji Misri katika mchezo utakaopigwa saa moja usiku ukitanguliwa na mchezo kati ya Kenya na Sudan.
Akizungumza kwa simu akiwa njiani jijini Nairobi, Kenya kwenda nchini huko, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Silyvester Marsh, alisema timu yake ipo katika hali nzuri kutokana na maandalizi waliyofanya.
"Kwa sasa (jana asubuhi), ndio tumefika Nairobi kwa ndege ya Shirika na Ndege la Misri na muda si mrefu tutaanza safari ya kwenda huko, kila kitu kinakwenda vizuri na wachezaji wapo katika morali ya juu kucheza mashindano hayo," alisema Marsh.
Wachezaji walioondoka ni makipa Juma Kaseja, Shaaban Kado na Said Mohamed, mabeki ni Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasyika, Nadir Haroub 'Cannavaro', Aggrey Morris, Kelvin Yondan na Juma Nyosso.
Viungo ni Nurdin Bakari, Shaaban Nditi, Jabir Aziz, Rashid Gumbo na washambuliaji ni Salum Machaku, Nizar Khalfan, Godfrey Taita, Athuman Machupa, Jerry Tegete, Ali Ahmad Shiboli na Said Maulid 'SMG'.
Mashindano hayo ni maalum kwa ajili ya kudumisha uhusiano miongoni mwa nchi zinazotumia maji ya mto Nile.
Nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ethiopia na Eritrea zitashiriki michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment