04 January 2011

Osiah, Wambura kuanika mikakati yao kesho

Na Zahoro Mlanzi

KATIBU Mkuu mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah na Ofisa Habari wake, Boniface Wambura, kesho wanatarajia kuanika mikakati
na malengo yao katika kuliongoza shirikisho hilo.

Viongozi hao walipata nafasi hizo baada ya kuteuliwa na Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, na kuwapiku wengine 64 walioomba nafasi ya ukatibu na 44, uofisa habari.

Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam jana baada ya kuanza kazi rasmi, Osiah alisema anashukuru kwa kupata nafasi hiyo na pia kwa saa chache alizokaa ofisini humo, amepata ushirikiano mzuri kwani alipokelewa vizuri.

"Tumeanza kazi rasmi leo (jana) na mwenzangu (Wambura), lakini bado hatujakabidhiwa ofisi rasmi kwa maana ya makabidhiano ya document (nyaraka), kwani aliyekuwa akikaimu ameondoka," alisema Osiah.

Alisema Kayuni (Kaimu Katibu Mkuu) ,ameisindikiza timu ya Taifa 'Taifa Stars' kwenda Misri na atakaporudi atakuwa na mapumziko kwani amekuwa akikaimu nafasi hiyo kwa muda mrefu, hivyo atakaporudi,  makabidhiano yatafanyika.

Alisema pamoja na hayo, kesho wataanika mikakati yao na mipango katika kuliendeleza soka la Tanzania,  ambapo watatoa na taarifa nyingine na jinsi watakavyofanya kazi.

Viongozi hao wameingia madaraka baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Fredrick Mwakalebela kung'atuka madarakani kwa kuamua kujiingiza katika siasa na aliyekuwa Ofisa Habari, Florian Kaijage, kusimamishwa, lakini mkataba wake ulikuwa umemalizika.

Osiah ana Shahada ya Sayansi ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amehudhuria kozi nyingi katika taaluma yake ya uandishi wa habari, pia alikuwa Mhariri wa Habari wa magazeti ya Mwananchi.

Kwa upande wa Wambura, ni msomi wa Shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, na Stashahada ya Tasnia ya Habari, amehudhuria kozi mbalimbali za uandishi wa habari na pia alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo leo.

No comments:

Post a Comment