Na Zahoro Mlanzi
WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Simba inatarajia kutua nchini leo ikitokea Komoro huku wakijuta kuwadharau
wapinzani wao, Elan de Mitsoudje ya nchini humo.
Timu hizo zilikutana juzi kwenye mchezo wa awali wa michuano hiyo, ambapo zilitoka suluhu matokeo ambayo Simba hawakuyatarajia.
Akizungumza kwa simu jana kutoka Komoro Meneja wa timu hiyo, Innocent Njovu alisema wachezaji wake walicheza chini ya kiwango kutokana na kuonekana kuidharau timu hiyo, lakini walikuja kushtuka muda ulikuwa umekwenda.
"Inaonekana timu za Komoro zimebadilika sasa, hatukutarajia kama ingetoa upinzani ule na hilo nadhani wachezaji wetu watakuwa wamepata somo, ila nina uhakika kama wangejituma kama kawaida uwezo wa kushinda ulikuwepo," alisema Njovu.
Alisema walitarajia kurudi jana, lakini kwa ratiba za ndege hakukuwa na usafiri wa kurudi nchini, lakini kwa leo ipo hivyo hawana budi kurudi.
Njovu alisema mara baada kurudi wataendelea na programu yao ya mazoezi kama kawaida kwa ajili ya kujiandaa na michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba inatarajia kushuka uwanjani Februari 5, mwaka huu kuumana na Polisi Tanzania katika mfululizo wa michezo ya ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment