31 January 2011

Wanariadha kibao kushiriki Kili Martahon

Na Mwandishi Wetu

WANARIADHA nguli wa mbio za marathon kutoka nchi mbalimbali duniani, wako katika hatua za mwisho za maandalizi kabla ya kwenda Moshi kushiriki
awamu ya tisa ya mbio za Kilimanjaro Marathon, zitakazofanyika Februari 27, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana Rais wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Francis John alisema wanariadha mashuhuri kama vile Patrick Nyangero, Andrea Silvini, Daudi Joseph, Sarah Majah, Sarah Kavina na Banuelia Brighton wataungana na wanariadha na wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Nyangero alikuwa mshindi wa pili kwenye mbio hizo mwaka 2009, baada ya kumaliza mbio katika muda wa 02:15:35 huku, Silvini alikuwa mshindi wa tatu mwaka 2008 baada ya kumaliza katika muda wa 02:16:22. Banuelia alishinda mbio hizo kwa upande wa wanawake akimaliza katika muda wa 02:48:37.

Wanariadha wengine waliothibitisha kushiriki ni pamoja na Martin Sulle, Peter Sulle, Samwel Shauri na Mary Naali ambaye hivi karibuni alishinda mbio ya Vienna Marathon nchini Austria.

John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, ambao ndiyo waandaaji wa mbio hizo alisema nchi zaidi ya 35 zinatarajiwa kushiriki huku washiriki kutoka nje ya nchi wakitarajia kuwa zaidi ya 600 ukilinganisha na 500 wa mwaka jana.

Washiriki wa kigeni wanatarajiwa kutoka nchi za Afrika Kusini, Uingereza, Zimbabwe, Kenya, New Zealand, China, Canada, Marekani, Australia, Ufaransa na Italia. Kwa ujumla, zaidi ya wanariadha 5,000 wanatarajiwa kushiriki mbio hizo.

Naye Meneja wa bia ya Kilimanjaro ambao ndiyo wadhamini wakuu wa Kili Marathon George Kaviseha alisema mashindano hayo yameendelea kuwa kivutio na ni mashindano makubwa ya kimataifa ikiwa na zaidi ya chi 35 yanayoshiriki.

"Mbio hizi huvutia wanariadha mashuhuri wa kimataifa na kuwapa fursa wanariadha wa Tanzania kujipima na kupata uzoefu katika mbio ndefu,” alisema Kavishe.

Wadhamini wengine washirikishi katika mbio hizo ni Vodacom ambao wanadhamini mbio za kujifurahisha za kilometa, CFAO DT Dobie, KK Security, TanzaniteOne, TPC Sugar, Precisionair, Kilimanjaro Water, Bodi ya Utalii Tanzania na Tanga Cement.

No comments:

Post a Comment