Na Addolph Bruno
TIMU ya soka ya vijana wenye miaka chini ya 20, ya JKT Ruvu, imetinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Uhai, baada ya kuichapa Simba bao 1-0, katika mchezo wa robo fainali uliochezwa Uwanja wa
Karume Dar es Salaam, jana.JKT Ruvu imekuwa timu ya tatu kuingia hatua hiyo, ikitanguliwa na AFC Arusha iliyowatoa African Lyon kwa mabao 2-1 na Ruvu Shooting iliyowaondosha Yanga kwa mabao 2-1. Yanga iliaga michuano hiyo juzi, baada ya kuchapwa na Ruvu Shooting.
Mchezo huo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa, dakika ya tano Kelvin Chale wa Simba, alikosa bao la wazi baada ya shuti lake kudakwa na kipa Phelemon Ramadhani wa JKT.
Hata hivyo, mchezo huo uliingiwa na dosari dakika ya 20, baada ya mwamuzi Isihaka Mwalile, kumtoa katika eneo la uwanja kocha wa Simba, Seleman Matola, kwa kutoa lugha chafu.
Kitendo hicho kilionekana kuwachanganya wachezaji wa Simba, lakini waliendelea kulishambulia lango la wapinzani wao.
JKT ilikianza kipindi cha pili kwa kulisakama lango la wapinzani wao, na kufanikiwa kupata bao pekee katika mchezo huo, dakika ya 51, lililofungwa na Frank Domayo.
Bao hilo liliwazindua Simba na kujibu mashambulizi, lakini mabeki wa JKT walikuwa imara kuondosha hatari langoni mwao.Simba nusura ijipatie bao dakika ya 75, baada ya Chale kupiga mpira juu na kutoka nje ya uwanja.
Mashindano hayo yataendelea kesho hatua ya nusu fainali, kwa mchezo kati ya AFC dhidi ya Ruvu Shooting na JKT itacheza na mshindi wa kati ya Mtibwa na Polisi Tanzania.
No comments:
Post a Comment