07 January 2011

Papic agoma kuchukua hati ya mkataba

Na Zahoro Mlanzi

KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Kostadin Papic, amegoma kuchukua hati ya mkataba mpya kwa kile kinachodaiwa, hana mpango tena wa kuendelea kuinoa timu hiyo.Kitendo hicho kilitokea kabla ya timu hiyo haijakwenda
visiwani Zanzibar kucheza Kombe la Mapinduzi, ambapo uongozi wa timu hiyo ulikaa naye kujadili hatma yake klabuni hapo.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo, kililiambia gazeti hili Dar es Salaam jana, kwamba Papic alifanya mazungumzo na uongozi wa juu na kukubaliana kwa baadhi ya vitu, huku kuhusu mshahara wakishindwa kuafikiana.

"Unajua Papic amemaliza mkataba wake Yanga, na sasa hivi anaifundisha tu kama 'deiwaka' kwa maana hana mkataba, sasa Yanga wamsainishe, lakini aligoma kufanya hivyo," kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliendelea kusema kwamba, tatizo la kugoma kusaini mkataba mwingine, ni kutokana na kusikia taarifa kwamba, viongozi wanafanya mazungumzo na Kocha Fredy Felix 'Minziro',  aliyekuwa akiinoa Ruvu Shooting ambaye kwa sasa ameshatua Yanga rasmi.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llody Nchunga kuzungumzia suala hilo, alikanusha kwa kusema, Papic amesaini mkataba mpya, ila zile nakala za mkataba, ndizo ambazo hajazichukua mpaka sasa.

"Tumemalizana na Papic na ataendelea kuwa kocha wetu, hilo suala la kutosaini mkataba halipo,  ila mpaka sasa hajachukua nakala za mkataba alizosaini kutokana na siku aliyopanga kuchukua, ndiyo ilikuwa siku ya safari ya kwenda Zanzibar," alisema Nchunga.

Alisema kocha huyo pamoja na Minziro, wameanza kufanya kazi pamoja, na ana imani ushirikiano wao, utaleta matunda makubwa ndani ya Yanga.

No comments:

Post a Comment