Na Grace Ndossa
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imezitaka timu za afya za mikoa na wilaya kuchukua tahadhari kuhusu ugonjwa wa Homa ya Manjano kwa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa
wagonjwa na utoaji wa taarifa za kila wiki za magonjwa ya kuambukizwa.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es salaam jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Bladina Nyoni kutokana na Taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani kuhusu ugonjwa wa homa hiyo uliojitokeza Kaskazini mwa Uganda ambapo watu 48 wamepoteza maisha.
Alisema kuwa, kutokana na tahadhari hiyo serikali imeandaa timu za watalaamu vifaa na tiba na chanjo za kutosha, kukabilina na huo ugonjwa endapo utajitokeza nchini.
Pia kuimarisha usimamizi na ufuatilijia wa wagonjwa bila usumbufu usio wa lazima, kwa wasafiri wanaotoka nje ya nchi hasa katika vituo vya afya vya bandari, viwanja vya ndege na Mipakani.
"Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inachukua fursa hii kutoa tahadhari kwa wananchi wote hasa wale waliopo katika mikoa inayopakana na Uganda, (Kagera, Mara na Mwanza) kutoa taarifa wanapoona mgonjwa mwenye dalili za Homa ya manjano," alisema Dkt. Nyoni.
Alizitaja dalili hizo kuwa ni kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli pamoja na mgongo, mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kusikia kichefu chefu na kutapika, mwili kuwa na rangi ya manjano, kutokwa na damu sehemu za wazi kama mdomo, pua macho na tumboni.
Aliongezea kuwa wakati mwingine damu huonekana kwenye matapishi na kinyesi na hatimaye figo kushindwa kufanya kazi, ambapo kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa huo ni kati ya siku ya tatu hadi sita baada ya kuambukizwa.
"Ugonjwa wa manjano hauna tiba kamili ila una chanjo, wagonjwa waliozidiwa wanahitaji huduma ya karibu ambapo mgonjwa anatakiwa kuongezewa maji mwilini kwa kunywa au kuwekewa dripu, hivyo wananchi wanatakiwa kutoa taarifa mapema wanapoona dalili hizo,"alisema Nyoni.
Asante kwa taarifa.Tutazifuata na tutakuwa makini.
ReplyDeleteInaonyesha ni ugonjwa hatari sana.Sija juwa unaambukizwaje.Kwa dar ukija siitakuwa hatari jamani?
ReplyDeleteHasa wakati wa asubuhi na Jioni wakati watu wanaporudi majumbani.Namaanisha msongamano..!Mungu tusaidie tuepuke na hili balaa!