Na Benjamin Masese
SERIKLI imefunga rasmi operesheni ya malipo kwa waathirika wa milipuko ya mabomu iliyotokea Aprili 29, 2009 eneo la Mbagala Kuu katika kambi ya
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya muda uliotolewa kuwasilisha malalamiko yoyote kumalizika.
Taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa jana Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Fanuel Mbonde alisema kuwa tangu Septemba 28,mwaka 2010 walitoa tangazo la kuwataka waathirika kuwasilisha malalamiko yao kabla ya Oktoba 13, mwaka huo lakini hakuna aliyejitokeza.
Hata hivyo Bw. Mbonde alisema kuwa pamoja na kufunga operesheni hiyo bado wametoa nafasi kwa mwananchi yeyote anayeona kuwa na madai halali kuwasilisha madai yake kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Chiku Galawa ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya wa maafa hayo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa katika maafa hayo watu 26 walipoteza maisha na wakazi 9,704 waliathirika kwa kuharibiwa nyumba na vyombo vyao ambapo waathirika 636 walipata majeraha.
Bw. Mbonde alisema katika taarifa hiyo kuwa serikali ilichukua hatua mbalimbali za kurejesha maisha ya wananchi ikiwemo kutoa chakula, matibabu pamoja na kuhudumia mazishi kwa marehemu 26, fidia na kifuta machozi.
Alisema kuwa serikali ilitoa jumla ya sh.460,000,000 kwa ajili ya kuhudumia waathirika na kati ya fedha hizo sh. 60,000,000 zilitengwa kuhudumia mazishi na kifuta machozi kwa familia za askari sita wa JWTZ ambapo sh. 200,000,000 zilipelekwa kwa raia 20 na kiasi hicho hicho kilitumika kwa ajili ya huduma chakula, matibabu na makazi makazi ya muda.
Vile vile aliongeza kuwa katika milipuko ya awamu ya pili iliyosababisha watoto watatu kupoteza maisha serikali ilitoa sh. 30,000,000 kwa ajili ya mazishi na kifuta machozi kwa ndugu na sh. 84,266,000 kwa JWTZ kwa ajili ya kuwawezesha kutafuta masalia ya mabomu ardhini kazi inayoendelea hadi sasa.
Bw. Mbonde alisema serikali ilifanya tathmini ya hasara iliyosababishwa na milipuko ya mabomu na kubaini nyumba 9,519 zinahitajika kufidiwa kwa gharama tofauti zilizofikia sh.8,049,303,324 na hadi sasa maisha ya waathirika yamerudia katika hali kama ilivyokuwa awali.
Alisema hadi kufikia Disemba 2010 tangu kuanza kutolewa malipo Agosti 2009 jumla ya waathirika 8,183 walikuwa wamelipwa Sh.7,537,760,849 sawa na asilimia 86.
Bw. Mbonde alisema kuwa tathmini ya pili iliyoanza Februari 19, 2010 ilijumuisha waathirika 1, 438 waliolalamika kupunjwa fidia zao na waathirika wengine 601 walioachwa katika tathmini mbili za awali.
Alisema jumla ya sh.1,144,508,000 zilitumika kuwalipa waathirika 993 waliothibitika kustahili nyongeza ya fidia na sh.1,109,184,00 zilitumika kuwalipa waathirika 967 waliopunjwa awali.
Aliongeza kuwa kuna makundi mbalimbali ya waathirika yaliyofanyiwa tathmini wakiwemo waliosahaulika katika tathmini ya awali ambao hadi Disemba 2010 jumla ya sh.259,995,000 zimetumika kuwalipa.
Bw.Mbonde alisema kuwa katika awamu ya tatu waathirika wawili ambao walipata ulemavu wa kudumu kwa kupoteza mkono wa kulia na mwingine mguu walipewa jumla ya sh.5,000,000 kila mmoja.
Alisema kuwa pamoja na serikali kulipa fidia hizo bado imepokea malalamiko 2,575 na kati ya hayo malalamiko 1,900 ni ya kupunjwa fidia, 596 ya kusahaulika 25 walioumia na 54 ya kuharibiwa samani zao ambapo yote yanaendelea kuchambuliwa kupata uhalali.
Hata hivyo taarifa hiyo ilivilaumu baadhi ya vyombo vya habari kwa kuishutumu serikali kushindwa kusikiliza na kuyatatua malalamiko ya waathirika hao licha taarifa za utekekezaji wa kutolewa mara kwa mara na Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke.
No comments:
Post a Comment