31 January 2011

Babati bado hakujatulia, wawekezaji wajawa hofu

Na Peter Ringi, Babati

WAWEKEZAJI katika katika Bonde la Kiru wilayani Babati, mkoani Manyara wameeleza wasiwasi wa usalama wao na mali zao mbele ya Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya wilaya ikiongozwa na mkuu wa wilaya Bw. Ian Langiboli wakidai wapo tayari kuhama.

Hayo yamesemwa juzi na wawekezaji hao wenye asili ya Kiasia baada ya wenzao wawili kuchomewa nyumba viwanda vidogovidogo vya kutegeneza sukari guru pamoja na zana za kilimo vitu vlivyodaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Bilioni 10 kuteketezwa kwa moto.

Walidai kuwa tangu kuibuka kwa  mgogoro huo wa ardhi katika bonde hilo uliodumu kwa takribani miaka 20, umesababisha vifo vya wawekezaji watatu miaka 10 iliyopita na mpaka sasa serikali mkoani Manyara haijafanikiwa kutatua mgogoro huo, huku wakiendelea kupata hasara.

Akiongea na Majira mmoja wa wawekezaji Bw. Suresh Natan alisema anashangaa kufanyiwa uharibifu wa mali zake, kwani bali ugomvi huo unamhusisha mwenzake ambaye naye alichomewa nyumba na mali zake.

Mwekezaji mwingine Bw. Mukesh Orkadi alitaja mali zilizoharibiwa na kuteketezwa kuwa ni trekta 10 mazao yaliyopo ghalani, nyumba na samani zilizokuwemo ndani, zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni5 pamoja na kisima cha mafuta ya dizeli.

Wananchi hao wenye mgogoro wa ardhi na Bw. Orkad, mwishoni mwa mwaka jana waliandamana hadi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Babati wakidai hatma ya maisha yao imegubikwa na lindi la umaskini kutokana na kushindwa kuyamudu baada ya kuwekewa pingamizi la kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji na baraza la ardhi.

Wengine walioonesha wasiwasi wa kushindwa kuendelea kuwekeza katika bonde hilo la Kiru ni pamoja na Bw. Parbat Sisodia ambaye ni mmiliki wa kiwanda kidogo cha sukari na Bw. Babuu Hatia ambaye anamiliki kiwanda cha pamba cha Hanang cotton mills, huku wakiilalamikia serikali kushindwa kuwahakikishia usalama wao na mali zao.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa za awali toka kwa kamanda wa polisi mkoani hapa Bw. Parmena Sumary alisema jeshi hilo, limefanikiwa kuwakamata wananchi watano ambao hata hivyo hakuweza kuwataja majina.

2 comments:

  1. Serikali ilikuwa wapi miaka yote ishirini hadi mambo kufikia hapa? Kuweka wawekezaji kwa mabavu bila ridhaa ya wananchi hasa pale ardhi yao inahusika kuna hadhari zake. Tumeyaona ya Mbarali na kwingineko. Tujifunze kutokana na haya.

    ReplyDelete
  2. Hao wawekezaji nao wamewasaidia nini wananchi kwa miaka hiyo 20?
    Ukiona wananchi wanachukua sheria mkononi, ujue haki haikutendeka. Ni rahisi mwekezaji kujumlisha gharama ya vitu alivyopoteza kuliko kupiga gharama ya maisha na haki za wananchi zilizopotea

    ReplyDelete