Na Rabia Bakari
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba anatarajia kuongoza maandamano amani yaliyoandaliwa na
chama hicho, kupinga serikali kuilipa mabilioni ya fedha Kampuni hewa ya kufufua umeme ya Dowans.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Bw.Julius Mtatiro alisema kuwa maandamano hayo yanatarajia kufanyika Februari 7 mwaka huu.
Alisema na yataanzia Buguruni Malapa na kuishia Kidongochekundu, ambako viongozi wa kitaifa wa chama hicho watawahutubia mamia ya waandamanaji.
"Tumekwisha litaarifu Jeshi la Polisi juu ya maandamano haya kupitia barua yenye kumbukumbu namba CUF/AK/DSM/NKM/B/002/A2/2011/08 ya Januari 28 , 2011.
"Kwa hiyo tunatarajia Jeshi la Polisi halitajaribu kuhujumu maandamana haya ya amani kutokana na taarifa zake za kiintelijensia ambazo zimekuwa maarufu hivi karibuni,"alisema.
Alidai kuwa kuhusu mambo ya kiintelijensia hata wao wameyafahamu sasa, na hayahusiani na kukataza maandamano ya amani, kwa kuwa mambo ya kiitelijensia yanasisitiza amani, hivyo hawataona sababu ya polisi kuzuia.
"Haya mabilioni yakipotea, hata wenyewe mishahara yao haitaongezeka na hatuoni sababu ya wao kutaka kuwalinda watu wachache wanaoumiza hadi familia zao.
"Tunawajulisha Watanzania wote kuwa kutokana na kiburi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kutojifanya hawasikii kilio cha Watanzania ambao ndio walipa kodi, katika sakata la wizi wa mabilioni ya fedha kupitia kampuni hewa ya Dowans, iliyozaliwa na kampuni hewa ya Richmond, CUF tumeandaa maandamano makubwa kupinga malipo hayo,"alisema.
Aidha licha ya maandamano, katika mkutano huo pia, alizungumzia kuhusu matokeo ya kidato cha nne mwaka huu na kudai kuwa ni moja ya kielelezo cha hali duni ya elimu ya hapa nchini.
"Hii inatokana na ubishi wa serikali ya CCM ya kutotaka kushirikiaa na wadau wa elimu na vyama vya siasa kama CUF ambacho kimekuwa na sera nzuri pamoja na mipango thabiti ya kuinua elimu,"alisema.
Waliofanya mitihani ya kidato cha nne mwaka jana ni wanafunzi 441,426 sawa na asilimia 96.36 na watahiniwa 16,688 ambao ni sawa na silimia 3.64 ya watahiniwa wote waliosajiliwa hawakufanya mitihami ambapo kwa waliofanya nusu yao yaani wanafunzi zaidi ya 202,369 wamefanya vibaya sana.
Alisema kuwa mfumo wa elimu hivi sasa umegeuka mchakato usio na maana tena na haumuandai mtoto kupambana na mazingira yanayomkabili, bali yanamuandaa kuja kuwa mzigo, aliyeko shule ya msingi anasoma ili aende sekondari na akitokea sekondari aende chuo chochote hata kama hana lolote kichwani.
"Hivi sasa kuna aina tatu za shule hapa nchini, shule binafsi zenye huduma nzuri na uangalizi mzuri ambazo ada zake ni za juu sana na zinazolipa mishahara mizuri na marupurupu kwa walimu na kusababisha kuwa na walimu wazuri wanaofundisha watoto kufa na kupona.
"Watoto wanaosoma katika shule hizi ni wale wanaotoka katika familia za kitajiri hata kama ni yatima, nyingi kati ya shule hizi ni zil ambazo watoto hata kufua hufuliwa na watumishi maalum wa shule, huku ndiko nchi inaandaa viongozi muhimu wajao na watu watakaoshika nyadhifa muhimu katika nchini, watu watakaoshika njia za uchumi wa nchi, huku ndiko wamelundikana watoto wa vigogo ambao baba zao uhubiri ujamaa na kujitegemea, amani na utulivu,"alidai.
Alizitaja aina nyingine za shule kuwa ni za serikali zilizokuwa zikifanya vizuri miaka ya nyuma lakini kwa sasa hazifanyi vizuri tena kutokana na serikali kutowajali walimu wanaofundisha shule hizo, sambamba na ukosefu wa vifaa na vitendea kazi.
"Shule za uongozi wa awamu ya nne (Voda Fasta) ambazo hukusanya watoto wa masikini ambazo pamoja na serikali kuunda mikakati mingi mibovu, inayoishia kunufaisha wakubwa katika warsha na serikali kuunda mikakati mingi mibovu, ndizo zilizoongoza vibaya sana tena nyingine zikiwa na majina ya viongozi haki wake zao.
"Shule hizi hazina walimu, madawati, na vifaa muhimu, shule hazina maabara. nyumba za walimu, wanafunzi hawana hata mlo mmoja shuleni, hizi ni shule zilizolaaniwa na CCM, zina matatizo kedekede na watoto hujiandaa kufeli hata kabla ya mtihani,"alidai.
Alisema chanzo cha matokeo mabaya mwaka huu ni kutokana na kutoka katika familia masikini ambazo hazina msukumo toshelevu wa ufuatiliaji na usimamizi mzuri kwa mtoto.
Alidai kuwa tatizo lingine ni mfumo mbaya wa makusudi ulioweka na CCM ili kuhakikisha kuwa watoto wa masikini wanazidi kuwa masikini, na wale wa vigogo na matajiri wanazidi kuneemeka kwa elimu bora.
Alisisitiza kuwa japo serikali imeipinga ripoti ya Taasisi ya Twaweza, lakini ina ukweli mkubwa.
"Hata hivyo hadi wanamaliza shule ya msingi, mtoto mmoja kati ya watano hawezi kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili, licha ya kumaliza miaka saba ya elimu ya msingi, watoto hao wanaendelea kubaki mbumbumbu maishani mwao,"alisema huku akinukuu sehemu ya ripoti hiyo.
Bw. Mtataro aliitaka serikali kutumia zaidi ya asilimia 25 ya bajeti yake kila mwaka kuboresha sekta ya elimu kwa ujumla.
"Serikali haina budi kufanya marekebisho ya mitaala kwa kuzingatia zaidia umuhimu wa maudhui, muda wa kila somo, uwezo wa wanafunzi na fadia ya somo lenyewe.
"Mitaala ilenge kukuza lugha ya kiingereza na hivyo kuwaongezea wanafunzi uwezo wa kumudu vizuri masomo ya sekondari.Hii ina maana pia lugha ya kufundishia shule za msingi iwe kiingereza na kiswahili kifundishwe kama somo linalojitegemea ili kuwafanya watoto wayamudu vizuri masomo ya sekondari, vyuo na elimu ya juu ambako lugha kote lugha ya kufundishia ni kiingereza,"alisema.
Alimalizia kwa kusema kuwa ni ubabaishaji mkubwa wa kufundisha watoto masomo kwa kiswahili elimu ya msingi na ifikapo sekondari masomo hayo hayo wanakaririshwa Kiingereza, hali ambayo inafanya hadi watu wanamaliza vyuo vikuu hawajui lolote.
Mungu abariki maandamano yenu kama CCM wanajifanya vichwamaji kiwatokea pua kama Husein kule Misri wache ujinga wao.
ReplyDeleteHabari za kiintelijensia (yaani habari za kizushi) zinasema kuwa maandamano hayo yamebarikiwa na wanaintelijensia (wazushi) wa sisyemu kwa kuwa dini za vyama husika zinafanana.
ReplyDelete