27 January 2011

Serikali kutoa matibabu kisukari bure

Na Agnes Mwaijega

WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hadji Mponda amesema huduma za upimaji na matibabu kwa wagonjwa wa kisukari zitatolewa bure katika
hospitali, zahanati na vituo vya afya vya serikali.


Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kuthibiti ugonjwa huo Dkt Mponda alisema serikali itatumia itahakikisha wagonjwa wa kisukari wanapata matibabu kwa wakati.

"Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa usioambukiza lakini unaonekana kuwa ni tatizo kubwa nchini ndiyo maana serikali imeamua kusimamia na kutoa fursa kwa wagonjwa wote," alisema Dkt. Mponda.

Alisema kutokana na ugonjwa wa huo kuwa ni tatizo, serikali itasimamia na kuhakikisha huduma za matibabu kwa wagonjwa wa kisukari zinafika katika maeneo yote nchini.

Alisema ikiwa mgonjwa wa kisukari atatozwa fedha katika maeneo hayo atoe taarifa serikalini.

Alisema kuanzishwa kwa mradi huo kuna umuhimu mkubwa kwa sekta ya afya nchini na utasaidia kusambaza huduma za afya kwa watu wote kwa urahisi.

Mradi huo ambao ni utakuwa wa miaka minne unafadhiliwa na Wagunduzi wa Ugonjwea wa Kisukari Duniani(WDF) utagharimu dola milioni 2.3.

Alisema WDF kwa kushirikiana na serikali chini ya Chama Cha Kuthibiti Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA) itahakikisha huduma zinasambazwa nchi nzima tofauti na hapo awali. 

Dkt. Mponda alisema wizara yake inatoa elimu ili watu wasiyofahamu kuhusu ugonjwa huo wafahamu na kuhamasisha watu kwenda kupima ili wajue kama wanao au hawana.

 "Watu wengi hawafahamu kuhusu ugonjwa huu ambao unaongoza kusababisha vifo na wana imani potofu kwamba wanaokufa ni wenye pesa tu," alisema.

Alisema ana imani kwamba wananchi watafaidika na mradi huo kwa kiasi kikubwa na utapunguza vifo vya watu wanaokufa kwa ugonjwa huo.

Aliwashukuru wote wanaoshirikiana na wizara katika kuboresha sekta ya afya nchini.

No comments:

Post a Comment