19 January 2011

Samba la kibrazil laitesa Yanga

*Mchezo wao na Simba bureee

Na Zahoro Mlanzi

TIMU ya Atletico Paranaense kutoka Brazil, imeifundisha samba timu ya Yanga kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2, katika mchezo wa
kirafiki wa kimataifa uliopigwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hiyo ambayo ilichezesha wachezaji wengi vijana wenye wastani wa umri wa miaka 20, ilitakata kwa jinsi ilivyocheza ambapo ilimiliki mpira na kupiga pasi zenye uhakika.

Katika mchezo huo, Yanga ilianza kwa kupiga pasi nyingi ndani ya dakika 10 za kwanza lakini ilijikuta ikishtukizwa kwa shambulizi la nguvu dakika 13 ambalo lilizaa matunda kwa bao lililofungwa na Bruno Costa kwa shuti.

Baada ya kufungwa bao hilo Yanga ilitulia na kufanya shambulizi dakika ya 24 ambapo Davies Mwape nusura aisawazishie Yanga bao baada ya kupiga shuti lililotoka pembeni ya goli kutokana na krosi ya Nsa Job.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 31, Mwape aliisawazishia Yanga, baada ya beki Salum Telela kufanya kazi ya ziada kupanda mbele na kupiga krosi iliyomkuta mfungaji.

Kipindi cha kilianza kwa kasi ambapo dakika tatu tangu mchezo uanze, Atletico walifunga bao la pili lililofungwa na Jenison Brito kwa shuti baada ya wachezaji wa timu hiyo kuonana vizuri.

Atletico ikiwa bado ina furaha ya kufunga bao la pili, wakajifunga wenyewe kutokana na shuti lililopigwa na Telela kumzidi nguvu Costa na kujikuta akiiutumbukiza mpira wavuni akiwa katika harakati za kuokoa.

Yanga iliendelea kuliandama lango la Atletico na dakika ya 80, Mwape nusura aifungie Yanga bao la tatu baada ya kupiga shuti nje ya eneo la hatari lakini kipa aliliokoa na kuwa kona tasa.

Zikiwa zimebaki dakika 10 kabla ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, Jenision aliifungia Atletico bao la tatu akiunganisha krosi ya Edgar Junio ambaye alimpiga boto Godfrey Bonny na kupiga krosi iliyomkuta mfungaji.

Wakati huo huo, waandaaji wa mchezo huo wameamua kuondoa viingilio vya mchezo wa kesho kati ya Atletico na Simba ambapo sasa mchezo huo utakuwa bure.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Rais wa Kampuni ya Oil & Industries, Rahma Al-Kharoosi alisema wameamua kuondoa viingilio vilivyokuwepo ili mashabiki wajitokeze kwa wingi kupata burudani.

Pia aliongeza, endapo Simba itaifunga timu hiyo, hakuna shaka ataigharamia kwenda nchini Brazil kurudiana nao.Viingilio vilikuwa ni cha juu sh. 200,000 na cha chini sh. 5,000.

1 comment:

  1. hongera waandaji kwa kutoa ofa kwa simba, kazi kwao wajitume.

    ReplyDelete