Na Elizabeth Mayemba
MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga ameupiga 'stop' mkutano ulioutishwa na wanachama wake kesho kwa madai ya kuwa na maandalizi ya Ligi Kuu mzunguko wa pili.Akizungumza Dar es Salaam jana Nchunga alisema
, tayari ameshawaandikia barua wanachama hao ili waaghirishe mkutano huo mpaka utakapopangwa baadaye.
'Nimesikia kwamba kuna mkutano wa matawi, ambao ulitakiwa kufanyika kesho lakini nimewaandikia barua ili wauaghirishe kwa kuwa tupo katika maandalizi ya mechi zetu za Ligi Kuu, mzunguko wa pili na michuano ya kimataifa," alisema Nchunga.
Alisema pia kutakuwa na kikao cha Kamati ya Utendaji hivi karibuni, hivyo kutakuwa na mambo mengi ambayo yataingiliana na amewataka wanachama hao wawe na subira mpaka hapo baadaye.
Jana baadhi ya magazeti yalimripoti Mwenyekiti wa Matawi ya klabu hiyo, Mohammed Msumi akisema kuwa, kutakuwa na mkutano wa dharura ambao umeitishwa kujadili uteuzi wa mdhamini mpya wa klabu hiyo aliyetangazwa Abbas Mtemvu.
Ajenda nyingine ni kuhusu malumbano ya mara kwa mara baina ya Nchunga na Makamu wake, Davis Mosha.
Hata hivyo imedaiwa kuwa kuna baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, wamepinga vikali mkutano huo kwa madai kwamba Mwenyekiti huyo wa matawi aliyeitisha hawamtambui kwa kuwa tayari alishamaliza muda wake.
No comments:
Post a Comment