10 January 2011

Pwani kujengwa uwanja soka wa kisasa

Na Masau Bwire, Kibaha

HATIMAYE ujenzi wa uwanja wa soka wa kisasa mkoani Pwani utaanza mapema mwezi huu mara baada ya jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja huo kutarajiwa kuwekwa Alhamisi wiki hii.Jiwe hilo la msingi pamoja na uzinduzi wa
kuanza kwa ujenzi utafanywa na Mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa Tanzania (JKT), Major General Samwel Kitundu.

Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Kikosi cha jeshi cha JKT Ruvu, Kanali Thomas Mbele alisema mara baada ya kuwekwa jiwe hilo la msingi ujenzi utaanza mara moja wakihitaji kuukamilisha mapema ili msimu ujao wa ligi uweze kutumiwa na klabu zitakazoshiriki Ligi Kuu bara.

Mbali na kukishukuru Chama cha Soka mkoa wa Pwani (COREFA), chini ya Mwenyekiti Hassan Othman 'Hassanol' ambacho alisema kimekuwa mstari wa mbele kwa mchango wa mawazo na mali kuhakikisha uwanja huo unajengwa, Kanali Mbele ametoa mwito kwa wadau wa soka na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kuchangia ujenzi wa uwanja huo.

"Naipongeza sana COREFA kwa kushirikiana nasi kwa karibu katika ujenzi wa uwanja huu ambao mbali na kutoa ushauri wa kitaalam tayari wamechangia mifuko 300 ya saruji na kiasi kikubwa cha fedha" alisema Kanali Mbele.

Kanali Mbele alisema kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo itakuwa faraja siyo tu kwa wakazi wa mkoa wa Pwani bali kwa Watanzania wote kwani ni uwanja ambao utatumiwa na Taifa kwa michezo ya kitaifa na kimataifa.

"Uwanja huu hautakuwa wa mkoa wa Pwani tu, ni wa watanzania wote hivyo mtu kama ana saruji, nondo, misumari, fedha taslimu au chochote kinachohitajika katika kukamilisha uwanja huu basi ajitokeze," alihimiza Kanali Mbele.

Alisema gharama na mahitaji halisi ya ujenzi wa uwanja huo ambao ramani yake imechorwa na Makao Makuu ya JKT kitengo cha upimaji, michoro na ramani zitatolewa baadaye mara ujenzi huo utakapozinduliwa.

No comments:

Post a Comment