LOME,Togo
SERIKALI ya Togo imesema kuwa majadiliano yanaendelea kati yao na Serikali ya Angola ili kulipa fidia kuhusu shambulizi dhidi ya timu ya Taifa ya nchi hiyo lililotokea katika Jimbo la Cabinda mwaka mmoja uliopita.Katika shambulizi
hilo, Kocha Msaidizi, Abalo Amelete na Ofisa Habari, Stanislas Ocloo waliuawa huku baadhi ya wachezaji na maofisa wengine wakijeruhiwa vibaya,
Kumekuwepo na lawama mbalimbali kutoka kwa waathirika wa shambulizi hilo kuhusu kukosa msaada kutoka pande zote mbili.Lakini hata hivyo juzi Waziri wa Michezo wa Togo, Christophe Tchao alisema kuwa kwa sasa wapo kwenye majadiliano ili kuweza kulipa fidia waathirika hao.
"Angola inataka kuandaa utaratibu wa kuwalipa fidia waathirika," Tchao .Tchao alilithibitishia Shirika la Utangazaji la Uingereza kuwa wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo na maofisa hao kwanza walikatiwa bima kabla ya kuanza safari ya Angola.
Waziri huyo alisema kuwa kupitia bima hizo, familia na waathirika wa shambulizi hilo walishakabidhiwa kati ya dola 10,000 hadi 25,000 kwa ajili ya kupoteza ama majeraha waliyoyapata katika shambulizi hilo la Cabinda.
Alikana taarifa za kwamba mlinda mlango, Kodjovi Obilale,ambaye amebaki na kilema cha maisha baada ya kushambuliwa kuwa ametelekezwa akisema kwamba malipo muhimu ya awali alishakabidhiwa na kwa sasa wanaandaa malipo mapya kwaajili ya mwaka huu.
"Serikali ya Togo kwa kushirikiana na Shirikisho la soka zinaandaa mpango wa kumpa usaidizi wa kifedha Obilale katika kipindi cha mwaka huu wa 2011,"alisema.
No comments:
Post a Comment