03 January 2011

Phiri aipa uzito Mapinduzi

Na Julius Kihampa

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, ameitaja michuano ya Mapinduzi kama moja ya kipimo sahihi kwa timu yao kwa ajili ya maandakilizi ya Ligi Kuu na Klabu Bingwa Afrika.Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Bara,  wakiongoza
katika msimamo msimu huu, wanatarajia kuvaana na timu ya Comoro kabla ya kuvaana na TP Mazembe, katika raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika msimu huu.

Akizungumza kutoka visiwani Zanzibar, Phiri alisema kikosi chake hakijaathirika kwa kiasi kikubwa na kushindwa kufanya vizuri katika michuano hiyo,  pamoja na kuondoka kwa baadhi ya wachezaji.

Alisema kila mchezaji aliyesajiliwa na katika timu hiyo, wameonesha kuiva na kusbiri kufanya vizuri katika michuano hiyo ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kusherehekea kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar.

"Kwa sasa inaweza kuonekana kama ni kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu, lakini naweza kusema ni pamoja na Klabu Bingwa, hasa kutokana na aina ya timu ambazo tutakutana nazo.

"Kuna timu kama Yanga, Azam, Zanzibar Ocean View, Mtibwa zote zina uzoefu mkubwa wa kucheza michuano ya kimataifa, hali ni nzuri kwetu na tunaamini tutafanya vizuri," alisema Phiri.

Nae, Meneja wa timu hiyo, Innocent Njovu, alisema lengo lao siyo kucheza fainali, bali kurudi na kombe hilo ili kuwahakikisha kuwa, kikosi chao kinaweza kufanya maajabu katika michuano yoyote.

"Tunataka kufika fainali, lakini lengo si kucheza tu mchezo huo, bali kurudi na heshima tunayostahili ya kunyakua kombe hili, hakuna mgonjwa mpaka sasa, na yeyote atakayepewa nafasi na mwalimu, anaweza kucheza bila wasi," alisema Njovu.

Simba itawakosa wachezaji walioko katika kikosi cha timu ya Taifa 'taifa Stars', kitakachoshiriki michuano ya Mto Nile ambao ni kipa Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Juma Nyosso na Mohamed Banka.

No comments:

Post a Comment