03 January 2011

Meya aanza kula na wazembe Songea

Na Mhaiki Andrew, Songea

MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Bw. Ally Manya ameanza kazi kwa kukemea watumishi waotelekeza ofisi na kwenda kufanya shughuli binafsi, huku wakiwaacha wananchi wakiangaika kutafuta huduma.Meya
huyo ameingia madarakani baada ya kumshinda Meya wa zamani, Bw. Gerald Ndimbo, diwani wa Kata ya Ruhuwiko, ambaye aliongoza manispaa hiyo kwa miaka mitano iliyopita.

Bw. Manya katika kikao chake cha kwanza kilichofanyika wiki iliyopita na wakuu wa idara wote wa manispaa hiyo alisema kuwa wakati umefika wa kuhakikisha kila kiongozi anawajibika katika sehemu yake ya kazi kwa kufanya kazi kwa umakini na bidii bila kumwonea aibu mtumishi mzembe.

Alisema tabia ya uzembe kazini ilikuwa ikisababisha kero nyingi ambazo zilikuwa zikitolewa na wananchi, ambao waliokuwa wakifika kutafuta huduma na kubakia wakipoteza muda mwingi kusubiria bila mafanikio.

Meya huyo ambaye diwani wa Kata ya Lizaboni, pamoja na kuwamwagia cheche wakuu wa idara aliwaonya watumishi wa idara ya ardhi ambapo alisema wamekuwa wakichangia kuwepo kwa malamiko ya mara kwa mara ya kugombea viwanja baada ya kiwanja kimoja kuwapimia wateja zaidi ya watatu.

Alisema kila mwananchi anahaki na uhalali wa kuhoji na kujua haki yake ya kisheria, badala ya kubakia kuwadanganya kila kukicha njoo kesho, njoo kesho, kufuatilia haki yake ambayo inaonekana ipo wazi kwa kuzingatia mikataba yake ya kisheria.

Katika kuhakikisha utendaji wa kazi kwa kila idara unakuwa na ufanisi wa kutosha aliwataka wakuu wa idara wawe na utaratibu wa kusikiliza maoni mara kwa mara kutoka kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment