07 January 2011

Dereba Abood asomea mashtaka 51

Na John Gagarini, Kibaha

DEREVA Maulid Mohamed (36) wa basi la Kampuni ya Abood ambalo lililosababisha ajali Januari 5, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi 49 amefikishwa mahakama ya wilaya ya Kibaha akishtakiwa kwa
makosa 51 ilikiwa ni pamoja na kuendesha gari kwa uzembe.

Dereva huyo mkazi wa mkoani Morogoro alisomewa mashtaka hayo kwa hakimu mkazi wa wilaya, Bi. Bahati Ndesarua, mbele ya mwendesha mashtaka, Bw Silas Jonas.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa katika eneo la TAMCO Mjini Kibaha, dereva huyo aliendesha gari kwa uzembe na kusababisha ajali iliyosababisha vifo vya mwendesha pikipiki na abiria wake.

Ilielezwa kuwa mwendesha pikipiki ambaye kwa sasa ni marehemu ni Bw. Hamis Dadi na abiria wake, Bi. Lucy Mageuza ambaye alikuwa mfanyakazi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Idara ya Ardhi.Dereva huyo alikana mashtaka hayo na kesi yake imepangwa kutajwa tena Januari 24, mwaka huu.

Ajali hiyo ilitokea Januari 5 mwaka huu baada ya basi la Abood lenye namba za usajili T 588 AYM lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro liliigonga pikipiki yenye namba za usajili T 616 BLF iliyokuwa ikikatisha kwenda Halmashauri ya Mji wa Kibaha baada ya harakati ya kutaka kuikwepa pikipiki hiyo kushindwa.

No comments:

Post a Comment