03 January 2011

Mwanafunzi mbaroni kwa kubaka mwenzie

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kishimba wilayani Kahama kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa shule ya msingi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 11.Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani alimtaja mwanafunzi kuwa ni Frank Stephano (16) mkazi wa mjini Kahama na kwamba tukio hilo lilitokea juzi saa 1.30 usiku.

Kamanda Athumani alisema mtuhumiwa huyo alifanya unyama huo baada ya kumvamia mwanafunzi huyo wa kike  (Jina na shule vimehifadhiwa) aliyekuwa katika matembezi ya kusherehekea mwaka mpya huko katika kitongoji cha Nyasubi mjini Kahama ambapo
alianza kumbaka kwa nguvu.

Hata hivyo alisema mwanafunzi huyo alipiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa wapita njia ambao walifika na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa ambapo walimpeleka katika kituo cha polisi cha mjini Kahama.

Tunamshikilia mtuhumiwa huyo na baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tukio hilo tutamfikisha mahakamani kujibu shtaka la ubakaji, tunawashukuru wananchi waliowezeshwa kukamatwa kwake na kumfikisha mikononi mwa vyombo vya dola pasipo kujichukulia sheria mkononi,alieleza Bw. Athumani.

Katika tukio lingine, polisi wilayani Bukombe inamshikilia mkazi wa Wilaya ya Chato mkoani Kagera kwa kosa la kupatikana na pikipiki inayohisiwa aliipata kwa njia za wizi.

Kamanda Athumani alimtaja mtuhumiwa anayeshikiliwa kuwa ni Bw. Elius Joseph (25) mkazi wa Chato ambaye alikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita saa saba usiku akiwa na pikipiki aina ya SANLG yenye namba za usajili T. 896 BCM.

Alisema polisi waliokuwa doria huko katika Kijiji cha Runzewe walimkamata mtuhumiwa huyo ambapo alipotakiwa kutoa maelezo juu ya uhalali wa kumiliki pikipiki hiyo alishindwa kufanya hivyo na hivyo kukamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

No comments:

Post a Comment