Na Sammy Kisika, Sumbawanga
WATU sita wamejeruhiwa na nyumba 13 kuezuliwa na zingine kubomolewa katika kijiji cha Miangalua wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa kutokana na mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha juzi kijijini hapo kwa takribani
saa moja.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Bw. Alfredy Ullaya, tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni, ambapo mvua ya mawe ilianza kunyesha kwa kasi kisha kufuatiwa na upepo mkali, kiasi cha kutia hofu kwa wakazi wakijiji hicho.
Bw. Ullaya alisema baada takribani dakika 15 kupita upepo huo ulizidi kuongeza kasi hivyo kuanza kuezua mapaa na kubomoa baadhi ya nyumba kijiji huku wananchi wakiwa ndani na kusababisha baadhi yao kuumia na kulazwa katika Zahanati ya Kijijiji hicho.
Aliwataja watu waliojeruhiwa na kulazwa katika zahanati hiyo kuwa ni Tatus Milumba, Rozina Changa, Joachimu Suwi, Emma Suwi, Samson Suwi na Harid Suwi ambao wamejuruhiwa katika sehemu mbalimbali za miili yao.Bw. Ullaya alisema hadi sasa wananchi hao wamehifadhiwa kwenye nyumba za jamaa na majirani zao wakati wakisubiriwa msaada wa serikali.
Wote waliokosa makazi na walioumia wanahudumiwa na ndugu na jamaa zao, kwani hadi sasa viongozi wa serikali hawajafika na kutoa msaada wowote,รข€ alisema Ullaya.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu Diwani wa Kata ya Miangalua, Bw. Msemakweli Sindani alisema kuwa amepata taarifa za maafa hayo na tayari alimwagiza Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho kuandika taarifa ya maafa hayo na kuipeleka kwa Mkuu wa Wilaya hiyo ili kamati ya maafa itembelee kijiji hicho na kufanya tathimini.
Hili ni tukio la tatu kutokea mkoani Rukwa katika kipindi cha miezi mitatu tangu msimu huu wa mvua uanze.
No comments:
Post a Comment