03 January 2011

Hoja ya Mnyika yasubiri tamko la serikali

Na Grace Michael

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, Bw. John Mnyika amesema kuwa anasubiri ufafanuzi wa serikali kuhusu suala zima la katiba ikiwemo muundo wa tume, hadidu za rejea na kama serikali itapeleka bungeni mapendekezo kuhusu mchakato kabla
ya kutoa kauli kuhusu hatma ya hoja yake binafsi ambayo alitarajia kuiwasilisha bungeni.

Alisema kuwa wakati akisubiri ufafanuzi wa serikali ambao inapaswa kuuweka hadharani, ataendelea na hatua ambazo alizitangaza katika uwasilishaji wa taarifa ya hoja yake Desemba 27, mwaka jana.

Taarifa iliyotolewa jana na mbunge huyo ilisema kuwa kutokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete, atatumia wiki ya kwanza ya Januari kukutana ana kwa ana na baadhi ya viongozi wa asasi za kiraia, taasisi za dini na vyama vya siasa ikiwemo CHADEMA ili kushauriana hatua za ziada za kuchukua.

Kama nilivyoeleza awali, hoja hiyo pamoja na kuwa inaitwa hoja binafsi kwa kanuni za bunge na mimi ni mwakilishi, lakini ni ya umma kwa sababu katiba mpya ni hitaji la wananchi, hivyo maamuzi kuhusu hatma ya hoja husika yatafanywa kwa kushauriana na wananchi na wadau wengine baada ya kupata ufafanuzi wa serikali,รข€ alisema Bw. Mnyika.

Alisema kuwa kabla ya wananchi kuanza kutoa maoni kuhusu maudhui, alitoa mwito kwa wadau wote kujadili kwa kina mchakato wa katiba mpya kwa kuwa mchakato usipokuwa sahihi hata maoni mazuri yakitolewa yanaweza yasifikie hatua ya kufanyiwa kazi kwa ukamilifu na hatimaye kukosekana tija ambayo inakusudiwa kwa kuandikwa kwa katiba mpya miaka 50 baada ya uhuru.

Bw. Mnyika alikumbusha kuwa mwaka 1991 chini ya uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi iliundwa tume ya kuhusu mfumo wa vyama Tanzania tume hiyo ilikuja na mapendekezo mengi ikiwemo la kutaka kuandikwa kwa katiba mpya, lakini serikali ilichukua machache ikiwemo la kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, hivyo mchakato unaotarajiwa kuanza sasa ungeshakamilika miaka mingi kama mapendekezo ya wakati ule yangetekelezwa kwa ukamilifu wake.

Tukumbuke mwaka 1998 Rais Benjamin Mkapa aliunda Tume ya Marekebisho ya Katiba, hata hivyo sehemu kubwa ya mapendekezo ya Tume hayakutekelezwa. Na Rais wa wakati huo aliikataa hadharani sehemu kubwa ya taarifa yao na kutangaza kuwa tume imefanya kazi kinyume na hadidu rejea.

"Wakati huo tume ilielezwa kuwa ilikwenda kinyume na maoni ya wananchi lakini kimsingi ni kwamba mapendekezo ya tume yalikwenda tofauti na misimamo ya serikali, hivyo ni lazima kujipanga katika kutekeleza suala hili, alisisitiza.

Alisema kutokana na mazingira hayo ni muhimu kwa mchakato wa sasa kufanyika kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na kuwekewa utaratibu bayana ikiwemo kuitaka tume yoyote itayoundwa kutumia mfumo wa 'Green Paper' ili wananchi wenyewe kuanza kutoa maoni yao kuhusu masuala wanayoyaona kipaumbele badala ya kuathiriwa kimsimamo na serikali au tume yenyewe.

Alisema kuwa pamoja na Rais Kikwete kuweka bayana kuwa tume anayoiunda itahusisha wadau, hata hivyo ni muhimu tume ikaundwa katika mfumo ambao ni shirikishi, sio tu wajumbe kuteuliwa kutoka sekta au kada fulani, bali pia kuwe na mashauriano kati ya kada au sekta husika kabla ya uteuzi ili kuwe na uwakilishi badala ya wahusika kujiwakilisha wenyewe au kumwakilisha aliyewateua.

Bw. Mnyika alisema kuwa anatambua tofauti aliyoionesha Rais Kikwete kwenye jambo hili kwa kutambua haja ya katiba mpya kinyume na kauli za watendaji wake ndani ya serikali, zikiwemo za Waziri Celina Kombani, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadaye Mwanasheria Mkuu, Jaji Fredrick Werema ambao wote walitaka marekebisho ya katiba kwa kuwekwa viraka mbalimbali.

1 comment:

  1. mnyika umefanya vema kuanza kusema ubabaishaji wa serikali za ccm. Wakati huu tuwe makini na ikiwezekana tuzipinge hata tume zenyewe maana uundwaji wake unaegemea kuibeba ccm badala ya masilahi ya Taifa. eli Arusha

    ReplyDelete