26 January 2011

Muungano kambi ya upinzani mashakani

*Mbowe awataka kina Hamadi Rashidi 'wazidi kusubiri'

Na Tumaini Makene

ZIKIWA zimebaki takribani wiki mbili kabla bunge la 10 halijaanza vikao vyake vya mkutano wa pili, hatma ya
vyama vyote vya upinzani kuwa na kambi moja rasmi bungeni, bado ni kizungumkuti, ikiwa vitaweza kuungana hivi karibuni kabla ya mkutano wa bunge ujao au hata baadaye.

Hayo yamefahamika ikiwa ni siku chache baada ya kamati ya wabunge wachache wa upinzani wasiokuwa katika kambi rasmi ya upinzani, kudai inasubiri majibu ya barua  waliyomwandikia Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe, wakiulizia uwezekano wa kuwa kitu kimoja kabla mkutano wa bunge haujaanza, Februari 8, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati ya wabunge hao wachache, Bw. Hamad Rashi Mohamed, 'kambi' yao inajumuisha Chama Cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi, United Democtratic Party (UDP) na Tanzania Labour Party (TLP).

Kwa sasa kambi rasmi ya upinzani bungeni inaundwa na Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya kutimiza masharti kama inavyoelekezwa katika Kanuni namba 14 (3) ya Kanuni za Bunge za mwaka 2007, inayosema kuwa ili chama cha upinzani kiweze kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni, lazima kiwe na asilimia 12 ya wabunge wote.  

Akizungumza na Majira jana juu ya hatma ya barua aliyoandikiwa, Bw. Mbowe alisema kuwa wabunge hao wanapaswa kuendelea kusubiri, kwani pande hizo zitaweza kuwasiliana kwa njia zilizo rasmi, si kupitia vyombo vya habari.

Alisema kuwa kwa sababu wabunge hao walimwandikia barua mkuu wa kambi rasmi bungeni kuulizia uwezekano wa vyama vyote kujumuishwa katika kambi hiyo, hawana haja ya kukimbilia kwenye vyombo ya habari, ilihali hawajui iwapo CHADEMA kimeshalijadili suala hilo katika vikao vyake au la.

"Kwa sasa siwezi kusema chochote kwa sababu suala hili si la Mbowe peke yake, suala hili lina process (taratibu) zake, wenzetu wasubiri majibu, sisi tutawasiliana nao kwa njia rasmi kama wao walivyotuandikia barua...hatuwezi kufanya maamuzi ya kisiasa kwa kupitia vyombo vya habari...la sivyo watu wanaweza kuwa wanatafuta cheap popularity.

"Hakukuwa na haja ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari, kama walinikosa mimi wangeweza kuwasiliana hata na naibu mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni...lakini CHADEMA bado hakijafanya maamuzi, wala si rahisi kufanya maamuzi haraka haraka tu kwa sababu watu fulani au vyama fulani wanataka.

"Wakati mwingine si sahihi wala si vizuri kufanya maamuzi kwa pressure (shinikizo)...suala hili siwezi kusema no (hapana) wala yes (ndiyo) lakini halihitaji haraka namna hiyo," alisema Bw. Mbowe.  

Mwishoni mwa juma lililopita, wakati wakizungumza katika mkutano wao na waandishi wa habari, kupitia kwa viongozi wao, mwenyekiti wao Bw. Hamad (Wawi-CUF) na katibu wa kamati hiyo Bw. David Kafulila (Kigoma Kusini-NCCR Mageuzi), walisema kuwa hatma ya wao kuwemo katika kambi rasmi ya upinzani inategemea majibu kutoka CHADEMA.

"Tumemwandikia barua mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe...mnakumbuka kuwa katika mdahalo wangu na yeye, yaani mdahalo kati ya mkuu wa kambi rasmi ya upinzani katika bunge la 9 na mkuu wa kambi wa sasa katika bunge la 10, Mbowe alisema kuwa suala hilo linahitaji mchakato wa vikao vya chama, hawezi kuamua mwenyewe.

"Tunaamini kuwa tangu wakati wa mdahalo huo, ambao uliandaliwa makusudi kwa nia ya kujadili mstakabali wa upinzani bungeni kwa lengo la kuwa na kambi moja inayojumuisha vyama vyote kama ilivyokuwa katika bunge la 9 lililoisha, CHADEMA watakuwa wameshakaa vikao na kuamua juu ya suala hili.

"Hivyo tumemwandikia barua mkuu wa kambi rasmi ili tujue tunakwenda vipi katika bunge linalotarajiwa kuanza hivi karibuni...tujue kama tunakwenda tukiwa wamoja au tutakwenda kama tulivyo sasa," alisema Bw. Hamad.

Hata hivyo, jana Majira lilipata habari kutoka kwa mmoja wa wabunge wa upinzani, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, lakini akionesha dhahiri kuwa suala la vyama vyote vya upinzani kuunda kambi moja rasmi bungeni, bado ni ndoto ya alinacha.

"Unajua watu hawataki tu kusema au kuweka wazi mambo mengine, hii ndoa yetu ya wapinzani wote kuwa pamoja ni suala gumu na tata kwa kweli. Upende usipende ushirikiano wa CUF na CCM katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar ni moja ya vikwazo hapa, ni ngumu mno.

"CUF wanapaswa kukubali kuwa faida waliyoipata kukubali kushirikiana na CCM huko Zanzibar ndiyo gharama ya wao kukosa uhalali wa kuonekana kuwa ni wapinzani wa kuaminika huku bara...kwa mfano hivi anapewa....(anataja jina la mmoja wa wabunge wa CUF) uwaziri kivuli wa mambo ya ndani, hivi atakuwa mtiifu kwa nani, kwa Mbowe au kwa Makamu wa Rais wa Kwanza, ambaye pia ni katibu mkuu wake.

"Achilia huo mfano, chukua mfano mwingine...hivi kwa mfano tunaingia sasa katika umoja, halafu mmoja wetu anawasilisha hoja binafsi inayogusa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, mfano suala la mabadiliko ya katiba huko yalivyovuruga katiba ya muungano, hivi wabunge wa CUF watasimamia wapi," alisema mbunge huyo.

Alienda mbali na kutoa madai kuwa CUF kinaviburuza vyama vingine katika kile kinachoitwa kamati ya wabunge wachache wasiokuwa katika kambi rasmi, "wanaburuzwa tu kama msukule akina...(anataja jina la mbunge mwenzake wa upinzani kutoka NCCR-Mageuzi), lakini hamna kitu pale, hata UDP na TLP hawamo mle, basi tu," aliongeza mbunge huyo.

Lakini pia tumaini la kamati hiyo ya wabunge wa CUF, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP, kuwa na kambi ndogo ya upinzani, limeonekana kutoweka baada ya Spika wa Bunge, Bi. Anna Makinda kunukuliwa na vyombo ya habari akisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za sasa za bunge, haiwezekani kuwa na kambi tatu bungeni.

Alisema kuwa CHADEMA walikuwa na sifa zote za kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa kuwa wana asilimia 12.5 ya wabunge wote, tofauti na vyama vingine vya upinzani, hivyo akavishauri vyama hivyo kuangalia uwezekano wa kuungana na CHADEMA.

Mabadiliko ya kanuni yalikuwa ni njia mojawapo ya kutaka kupata nafasi ya kutambulika, iwapo ile ya kuwaomba CHADEMA itashindikana "kwa kweli wakati tukibadilisha kanuni wakati ule tulijisahau kuangalia hili...si vizuri kabisa kukiacha nje ya kambi rasmi ya upinzani chama kingine cha upinzani chenye wabunge pia," alisema Bw. Hamad, huku akiungwa mkono na Bw. Kafulila katika mkutano wa mwishoni mwa juma.

Semina elekezi

Wakati huo huo, wabunge wa bunge la 10 wamekumbushwa kuwa wanao wajibu wa msingi katika maeneo manne, ambayo ni; katika majimbo yao ya uchaguzi, kwa nchi, kwa vyama vyao na kisha kwa dhamira zao wenyewe.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais Dkt. Ghalib Bilal wakati akifungua semina elekezi kwa wabunge wote jana Dar es Salaam, akiongeza kwa kutoa wito kuwa wanapaswa kuwa karibu na wananchi waliowachagua ili kwa pamoja waweze kutafuta majawabu ya kero mbalimbali zinazowakabili.

"Kwa kufanya hivyo mtakuwa mnatekeleza mojawapo ya kazi yenu muhimu-uwakilishi wa wananchi. Miaka mitano kuanzia sasa si mingi," alisema Dkt. Bilal.

Spika na hoja binafsi za wabunge

Naye Spika wa Bunge, Bi. Anna Makinda jana alisema kuwa hatakuwa na tatizo kwa hoja binafsi yoyote itakayowasilishwa ofisini kwake almuradi iwe imekidhi vigezo vya kikanuni kuiwezesha kujadiliwa bungeni, baada ya kuangaliwa na wataalamu.

Alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) juu ya mgawo wa umeme na sakata la kampuni tata ya Dowans, ambapo alisema mpaka sasa mbunge huyo bado hajawasilisha hoja yake hiyo mbali na kuwa tayari ameshawasilisha barua ya kusudio la kuwasilisha hoja.

"Ni muhimu mkaelewa mpaka sasa alichowasilisha (Kafulila) ni barua ya kusudio la kuleta hoja binafsi, si hoja binafsi...hivyo ni vitu viwili tofauti kabisa...lakini sina tatizo na hoja yake au ya mbunge mwingine yeyote, kinachotakiwa ikidhi kanuni za bunge tu...akileta tutakaa na wataalamu tutaifanyia kazi, ikiwa haina tatizo tutamwambia ajiandae kuiwasilisha," alisema Bi. Makinda.

Habari zilizopatikana jana jioni katika eneo la semina elekezi ya wabunge na kuthibitishwa na Bw. Kafulila, zilisema kuwa ofisi ya bunge imejibu barua ya mbunge huyo, ikimtaka awasilishe hoja yake ofisi za bunge, tayari kwa kufanyiwa kazi.

"Ndiyo nimepata barua hiyo, lakini ni ya siri, siwezi kukuonesha...lakini jibu la lini nitawasilisha hoja yangu ofisi ya spika siwezi kulisema sasa, labda kesho nitakuwa katika nafasi nzuri ya kusema," alisema Bw. Kafulila.

24 comments:

  1. mh siasa za bongo kaaaaaz kwelikweli lbd wachangiaji wenzangu nisaidieni ati suluhisho lake ni nini?

    ReplyDelete
  2. huyo mboe ni mtata chadema sio yake tatizo kubwa la huyo ndugu ni mbinafsi na makengeza yanamzingua

    ReplyDelete
  3. inachofanya chadema si sawa kuna leo na kesho sasa hivi wana asilimia 12.5 wameunda kambi rasmi ya upinzani peke yao.kesho itakuwa chama kingine wasije wakalia kinachoshangaza zaidi ni vyombo vya habari kushindwa kuikosoa chadema kwa hilo na badala yake hujikita kwa kusema wanayosifa ya kufanya hivyo. nakumbuka 2005 pale CUF ilipotaka kufanya hivyo na ikaandamwa na laiti kama si CUF kuwaingiza wenzao wa chadema isingefika hapa leo ilipo.kwa sababu upinzani unapotoa azimio kwa umoja wao huwa na nguvu na zile hoja zao za ufisadi zilikolezwa na sauti moja ya upinzani. kwa sasa naona kuna visasi kutokana na uchaguzi uliopita na nia mbaya ya baadhi ya vyama kwa vyama vingine labda suala la maslahi .hoja ya chadema kwamba cuf iko serikalini zanzibar haina mashiko si wanaweza kuweka kanuni za mshirikiano na atakaekwenda kinyume akaondolewa "automatic" hilo halisemwi hapa kuna nini?

    ReplyDelete
  4. Kwa Wazanzibari ni bora ibaki hivyohivyo msiwepo kwenye hiyo kambi kwa manufaa ya Zanzibar,umoja wa kitaifa Zanzibar una faida kubwa kuliko kuwa kwenye hiyo kambi ya upinzani,hao ni watu waliofaidika na migogoro ya Zanzibar iliyowafanya Wazanzibar kutokuwa wamoja kudai haki zao. enzi za DIVIDE AND RULE ZIMEKWISHA,UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR NI BORA KULIKO HIYO KAMBI NA KAMA WALICHOFANYA ZANZIBAR KIBAYA MBONA MKUU WENU ALIWAHI KUSEMA TUIGE ZANZIBAR WALIVYOFANYA?

    ReplyDelete
  5. Magazeti gani yaseme? magazeti na makanisa yao moja,chadema kwao ni malaika haikosei

    ReplyDelete
  6. Nilipata matumaini sana baada ya kuona chama shupavu kimefanya vizuri katika uchaguzi mkuu uliopita wa Rais na Wabunge. Kwa bahati mbaya CHADEMA hakijachukuwa nafasi ya Urais, lakini ina wabunge wengi. Hivi inalifanya Bunge la 10 kuwa Bunge ambalo si lele mama!

    Tunategemea mabadiliko makubwa ya kifikra na mkinzano mkubwa wa mawazo na hoja lakini pia hekima na busata kutawala ili kulinda heshima ya Taifa letu!

    Bunge la 9 chini chini ya kambi ya upinzani ya CUF ilifanya mema hasa kuleta maelewano na miongoni mwa vyama vyote vya siasa vya upinzani na pia hata chama tawala na serikali yake! CUF mnastahili pongezi kwa hilo! Mmeiacha nchi salama!

    Hoja nayotaka kuijenga naielekeza kwa Kambi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA chini ya Uenyekiti wa Freeman Mbowe! Tangu mbowe aingie madarakani manung'uniko kwa vyama vya upinzani nimeyasikia ya wazi kabisa, na pia wadau wengine wa siasa nao wametoa manung'uniko yao kuelekea kwa Mbowe na si CHADEMA!

    Wapo watu wanaomuunga mkono kuwa ni kiongozi shupavu, asiyetetereka na msimamizi mzuri wa hoja zake na hoja za chama chake! Lakini pia wapo watu wanaommwona kama mtu asiye na hekima, mshari, mbinafsi na mwenye kusimamia hoja zinazoleta utengano, hasa kwa wana siasa wenzake walio tofauti naye! Kwa ujumla wanamwona kama si mstahimilivu na mvumilivu wa mambo hasa yanapo muuma!

    Mimi sitaki kuamini haya, nataka kumwona Mbowe kama kiongozi shupavu, mwenye msimamo wa dhati dhidi ya ufedhuli wa viongozi wetu dhidi ya Rasilimali za Taifa. Mwana Mapinduzi wa kweli, nk!

    Ninachomwomba Mhe: Mbowe asiach watu wakaendelea kumtazama kwa upande ule mbaya hasa kwa kuendelea kuwakataa wapinzani wenzake kwa hoja dhaifu! Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yawe ni chachu imara ya kuleta mabadiliko ya katiba na utambuzi wa vyama vya upinzani vilivyo kwenye serikali ya umoja wa kitaifa ya Zanzibar!

    CUF hawaombi hisani au UDP, au TLP, au NCCR nk hawaombi hisani ya kuingia kwenye kambi ya upinzani Bungeni. Sisi kama watanzania Bara tunawatambuwa hawa kama viongozi wa upinzani huku bara na wanastahili heshima hiyo! Sasa kama CHADEMA mtawakatalia mtaongeza wigo wa watanzania wanaowafikiri kuwa ni tatizo!

    Wapo baadhi ya Watanzania wanafikiria hata kutafuna namna DR. Slaa arudi bungeni akatusaidiee Watanzania kuongoza kambi hii muhimu ya upinzani hasa katika kipindi hiki muhimu cha kuleta mabadiliko ya katiba na usimamizi bora wa maadili ya viongozi na rasilimali zetu! Lakini tusifike hapo bado tumwamini Freeman Mbowe kuwa anaweza na kwa suala hili la Collective Responsibility of the Opposition Parties ndani ya Bunge Mhe: Mbowe na CHADEMA wataamuwa kwa busara bila masharti yeyote kwa wenzao wa upinzani huku wakitazama kama kuna hindrances zozote za kisheria basi wawe na jukumu la pamoja la kuliondoa. tunahitaji sana upinzani wenye nguvu ili kulinda maslahi ya Taifa hili, kuleta uwajibikaji na kusukuma mbele maendeleo yetu kwa faida ya vizazi vijavyo!

    Nisingependa hili lishindikane, lakini hata likishindikana basi tutengeneza kanuni itakayoruhusu vyama hivi vya upinzani vinavyojiona vimetengwa kuwa na umoja wao wa Kiliberali ili watazame shilingi hii kwa pande zote mbili!

    Naamini CHADEMA na Mbowe hili hawataliafiki, kwani nachelea kusema watanzania hawatawaelewa! Mbowe na CHADEMA wanahitaji strong Opposition itakayojumuisha vyama vyote bila ubaguzi. Vikiamini upendo huu wa visiwani utastawi hata kwa bara muda ukifika na tumewatuma huko mkalisimamie hili ili tufike huko!

    By Carwin

    ReplyDelete
  7. Watanzania wenzangu tuache manung'uniko yasiyo na sababu. Mbowe kuwa kiongozi wa upinzani bungeni haina maana atakataa hoja za wabunge wa vyama vingine. Wanachotakiwa kufanya vyama ambavyo havipo kwenye kambi rasmi ya upinzani ni kumpasia mpira Mbowe. sidhani atakataa hoja ya upinzani wa kweli.

    Tatizo kubwa la vyama vingine ni kuona wao hawatasikika au kusikilizwa hoja zao. Mimi sio CHADEMA ila kwa mtazamo wangu CHADEMA ndio watakaowawakilisha wapinzani wote bungeni. Ni kama CCM inavyounda Serikali, mbona CCM hawakuwashirikisha CHADEMA kuunda serikali? Ni utaratibu tu unaotakiwa kufuatwa. Sio kuanza kuchonga tuu mradi Mbowe na CHADEMA waonekane wabaya.

    Halafu, heri mbunge wa CUF ya bara angekuwa anaomba kuingia upinzani. Hamad anang'ang'ania nini upinzani wakati anajua yeye wakati wowote Dr. Shein anaweza kumteua kuwa waziri? Anasubiri ateuliwa waziri ndio ajione yeye sio mpinzani? Acheni kutudanganya CUF. Mmchemsha kufunga ndoa na CCM. Hiyo inatosha kwa miaka hii mitano.

    Bwana Kafulila alishindwa kuvumilia kukaa pamoja na Mbowe CHADEMA, tunadhani watakaa kwa amani ofisi mmoja bungeni? Mambo mengine yanahitaji kuvumiliana tu. Hakuna mtu aliye kama malaika. Leo unaona udhaifu kwa mwenzako, lakini wewe ukipewa hiyo nafasi tutauona udhaifu wako pia.

    Tukubali kuongozwa na sheria zilizopo hadi tutakapozibadilisha. Bora tupiganie katiba mpya kuliko kuwapeleka Hamad na Kafulila kambi rasmi ya upinzani.

    Nawashauri CHADEMA kama mnafuatilia maoni ya haya MSILOGWE kuwaingiza hawa jamaa upinzani bungeni mpaka watuonyeshe kwa vitendo huku nje kuwa ni wapinzani wa kweli- kwa kuwaunga CHADEMA mkono kwenye hoja zenu. Tabia waliyoionyesha wakati wa kuchagua Spika inatosha kutuonyesha lengo lao. Ndio maana Makinda anawapigia debe.

    Tunachotaka ni HAKI kwa raia wote na si kila mtu awe kiongozi. CCM na CUF wameunda serikali, na CHADEMA waunde serikali kivuli, basi. Chonde chonde CHADEMA msituangushe.

    ReplyDelete
  8. Naomba CHADEMA waliangalie suala hili kwa kina na kutolea majibu yatakayokidhi matakwa ya watanzania kama hawataki kujiunga na wenzao watuambie sababu gani turidhike nazo na kama wanajiunga nao hali kadhalika waseme, ila siku zote umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu kazi kwenu

    ReplyDelete
  9. Hivi ingekuwa nyie CHADEMA hamkupata viti vingi kuliko wenzenu, si mngeomba kushirikiana na wenzenu au mngekaa peke yenu? kama mngeomba kama mlivyofanya 2005 ugumu uko wapi? mie sielewi nyie ndio viongozi na kiongozi atatoka kwenu mtawekeana CUF atafanya A, UDP atafanya B, NCCR atafanya C na TLP atafanya D akishindwa mtu kuendana na mlivyopangiana atatupwa nje kama ambavyo BWANA MAPESA alivyoondolewagwa kwenye uwaziri kivuli wakati wa bunge la 9, wananchi wangependa kuwaona mnaungana kwa misingi hiyo ili muweze kujenga kambi imara vinginevyo itakuwa hao wengine wanaunga mkono CCM kwenye hoja za kwenu kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa spika na naibu wake kura zenu CHADEMA mliwapigia wagombea wenu na za wale wengine zilienda CCM kwakuwa hamuwataki fikirini hicho ndicho mnachokitaka?

    ReplyDelete
  10. Kweli ndugu kama umeingia kichwani mwangu ukanikaba na kuninyanyanya wezo langu. Sasa hawa CUF watakuwa upande gani katika kura yao. Kura yao tulishaiona ipo CCM, sasa huku wanakolilia Chadema si kuleta vita na majungu ya kuvuruga upinzani? Sasa kura mpigie CCM na kuiunga mkono bungeni, halafu mseme kuwa nyinyi ni wapinzani kweli inawezekana kweli. Sasa mnaikosoaje hiyo CCM?


    CHADEMA bunge lililopita walikuwa sio kigeugeu kama nyinyi mlivyoonyesha kwa chadema madharau, na kuanza kulia mnabaguliwa, habari tulikuwa tunazifuatili sana. Mbowe tumemsikia aliwaita mara kibao mpaka Mh ZITTO akasema yupo tayari kuvua kofia yake ampe HAMADI lakini mkakazania kuunda kambi yenu ndogo.CHADEMA muwe macho sana yasije yakawafika yale ya Mrema na NCCR Mageuzi.


    Halafu watoa maoni mnamshambua Mbowe, mnampa lawama bila sababu yeye sio mtoa maamuzi mnafahamu Demokrasia ya CHADEMA jambo likishindikana linatupwa kwenye kura ya siri. Maoni yangu CUF, NCCR, TLP na UDP muwe wavumilivu Mbowe hawezi kukurupuka peke yake. Haya ni maoni yangu.

    ReplyDelete
  11. Nashukuru kwa wachangiaji wenzangu hapo juu hasa huyu wa mwisho kachangia vizuri bila ushabiki wa chama.
    Maoni yangu ni kwamba kama alivyosema Spika Anna makinda CHADEMA hawakufanya makosa kuunda kambi ya upinzani bungeni na walifanya hivyo kwa sababu ya kukidhi kanuni ya kutimiza 12% ya wabunge.
    Nikirudi kwenye hoja ya wabunge wa CUF kwamba ni wapinzani au ni viongozi walioshika hatamu.Makamo wa kwanza wa Rais Sheikh Sharif amad alisema wabunge wa CUF ni wapinzani kwenye bunge la Jamhuri ya muungano wa TZ.
    Nikirudi kwenye mdahalo kati ya Mbowe na Amad Rasid Mbowe alitoa mashart kwa CUF kuunga mkono kutomtambua Rais na kuundwa kwa katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi na CUF walikataa.
    Kwa muono wangu kwa utofautiano wa kimtazamo kama hiyo hata kambi ya upinzani ikiundwa kwa ushirikiano wa vyama vyote udhaifu wa kupingana wao kwa wao utakuwa mkubwa na ile dhana ya kuwa na upinzani imara haitakuwepo na udhaifu wa kambi ya upinzani utaonekana. Kumbuka CHADEMA wanamisimamo yao tofauti na vyama vingine hasa CUF na CUF walipinga hadharani ili mnalionaje wadau.
    Kotofautina na kupingana hadharani kulikuwepo kipindi cha uchaguzi watu kama akina mrema waliipinga CHADEMA na kusema ni heri CCM ichaguliwe kuliko kuchagua CHADEMA lakin hizo ni habari za uchaguzi zimepita.
    Mapendekezo yangu kama CUF wanashindwa kueleweka kama ni upinzani halisi au wanaweza kujumuishwa na kuangalia mwenendo wao na wakiwa nje ya msimamo wa kambi ya upinzani basi waondolewe kama alivyoondolea John Cheyo kwenye bunge la 9 baada ya kuunga mkono upande wa serikali wakati kambi ya upinzani ilipinga.
    Kama ikishindikana kuwajumuisha CUF basi wabunge wa NCCR-MAGEUZI wajumuishwe kwani sioni tatizo kwao mbunge kama Kafulila ni mtu makini atasaidia upinzani lakin mtu kama mrema atawasumbua haeleweki.
    Kwa leo ndio mchango wangu.

    ReplyDelete
  12. Hawa CUF bana hawaeleweki wapo upande gani. Na hawa ndio wanaochangia sana hili suala la udini na ukabila wala si CCM japokuwa CHADEMA wanasema ni CCM. Hapa tunatafuta ni nguvu gani itumike bungeni tayari watoa maoni wameshaanza kufurumua mambo ya dini, mtu binafsi haya yanatoka wapi.

    Chadema kuweni macho, hawa sio wa kukaachungu kimoja kwa maoni yangu. Ingekuwa CUF ya huku bara sana.

    ReplyDelete
  13. JAMANI WATANZANIA NAONA KAMA MMESHAPITWA NA WAKATI. SASA HIVI TULITAKIWA TUWE TUNAZUNGUMZIA MASUALA YA NAMANA YA KUTEKELEZA ZILE AHADI TULIZOTOA KWA WAPIGA KURA. JE, KINA MBOWE, MAKINDA, CUF, CHADEMA AU MAGAZETI KWA SASA HAVITUSAIDII CHOCHOTE HASA SISI WAKULIMA VIJIJINI LBDA NINYI MLIYO MIJINI WENZANGU. TUNASUBIRI KWA HAMU KUBWA MHESH. MAKINDA ATUAMBIE HOJA NZITO ZA KUWALETEA MAENDELEA ZINAZOTARAJIA KUTUWASILISHWA BUNGENI NI ZIPI. TUNATAKA HOJA NZITO ZA KUWAONDOA MAFISADI, KUONDOA KERO ZA UMEME, KUBADILI KATIBA NK. SIYO KLETA SIASA ZA KINA CUF, CHADEMA NK.

    ReplyDelete
  14. Mimi ni yule yule Hafidh - mpenda mageuzi na mwanaharakati wa kweli.napenda na mimi nichangie ktk hoja hii ya msingi lakini nitakua mwizi wa fadhila ikiwa sitampongeza ndugu yangu Carwin alietoa mchango mzuri sana kuliko wachangiaji wote naweza kusema hivyo.tunahitaji mawazo kama haya .Big up Carwin.
    Sasa niingie katika mchango wangu wa mawazo ktk hoja hii na jinsi watu walivyochangia. mimi ntagusia pamoja tuu amabapo nahisi wanachadema wana wasiwasi na hili. mana hata mbunge alienukuliwa na habari hii nae kasema anamushkeli na hili.tatizo wanaloliona wanachadema kua CUF na CCM kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar!!Mimi naona hii hoja haina msingi kwa sababu hii Serikali ni mhimili unaojitegemea na Bunge au Baraza la wawakilishi ni mhimili mwengine unaojitegemea.sasa ukiwa Mbunge au mwakilishi hata kama chama chako kinashika madaraka basi unayo haki yakuhoji serikali kwa maslahi ya taifa ndio kinachofanyika Zanzibar ktk baraza na hata katika Bunge la tisa mbona walikuapo wabunge wa CCM walioitoa kamasi serikali na kufika kutoa maneno makali kwa mawaziri.
    Kwa hiyo hii sio hoja kusema eti ukiwa chama chako kinaongoza Serikali basi usihoji.
    Sasa kwa mtazamo wangu Chadema waondoe masharti yasio na msingi na waunde Kambi moja ya upinzani ili iwe na nguvu bungeni kwa maslahi ya taifa.
    Pili napenda kuuliza hapa kama kuna mtu ana uelewa wa kanuni za Bunge anijibu - Jee ikiwa ktk Bunge kuna wabunge kutoka upinzani vyama viwili tofauti na wamefikisha idadi ya wabunge ambao wanaweza kuunda kambi ya upinzani itakuaje ? mana kwa mujibu wa mama Ana Makinda kua kanuni zinaruhusu kambi mbili tu ? naomba nijibiwe.

    ReplyDelete
  15. Acheni uhuni nyie CUF na NCCR.CHADEMA ndio chama cha upinzani.HAMADI Mwezi uja atateuliwa kuwa Waziri wa Viwanda Zanzibar.Lakini Hiyo CUF jamani Wabunge wake(ukimtoa Barwan) jamani siwanawakilisha Wazanzibar kambi ya Upinzani?Sasa upinzani wao wakufanyie hukohuko Zanzibar,Hapa kazi tuu kudadeki.Hatuwataki kwenye kambi yetu.

    ReplyDelete
  16. Hili suala la kuwa na wabunge kutoka Zanzibar limekuwa linanipa taabu saana. Hivi mbunge anayechaguliwa na wapiga kura 2000 anapata wapi legitimacy ya kulingana na mbunge anayechaguliwa na wanainchi 40000. Huu ni aina fulani ya usanii ambao watanganyika tumekuwa tukiuendekeza. CUF na wabunge wao kutoka visiwani hawana legitimacy ya maaamuzi ya bunge kuu la bara. katiba mpya inahitajika kurekebisha kasoro hii. Kutokana na hili, Chadema mnayo haki kimsingi ya kutohusisha wabunge kutoka visiwani. kuhusu ushirikiano na CCM, nadhani nalo liko wazi. kwamba, huwezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Chadema wasiwafikirie CUF katika kambi ya upinzani. Kwa wabunge wa upinzani kutoka Tanganyika, Chadema inaweza kuwashirikisha bila hata kufikiria, lakini waongozwe na ilani na msimamo wa Chadema.

    Nawatakia mema Chadema na Saa ya Ukombozi ni Sasa. (hii Slogan si vibaya kuanza kuitumia)

    ReplyDelete
  17. Tusifanye unafiki, Nyerere alisema siasa ni imani. Na kweli ni imani. na imani hii inakaa moyoni mwa mtu. Mtu mmoja hawezi kuwa na imani mbili moyoni na zote zikawa sawa. Huwezi kutuambia mbunge wa CUF anayetoka zanzibar atakuwa na imani mbili. moja: anaamini katika umoja wa kitaifa kati ya CUF na CCM na pili: aamini katika upinzani kati ya CUF na CHADEMA.
    Hizi imani mbili Umoja wa Kitaifa, na Upinzani zikianza kupingana ndani ya mioyo wa wabunge wa CUF watatupeleka kusikoeleweka.
    Katika hali ya kawaida, chukua rangi ya kijani (CCM) changanya na rangi za CUF na za CHADEMA, utapata rangi gani?

    Tuache ushabiki wa kuoneana haya. Wabunge wa CUF zanzibar wanaamini katika Umoja wa kitaifa kati ya CCM na CUF. na sisi hatujui walichokubaliana mpaka wakapendana hivyo. Tusiwaingize kwenye imani walioikataa ya upinzani, hata kama wanaililia. Hata wa bara pia wameridhia makubaliano ya Zanzibar, hawafai kuwa wapinzani.

    Wengine kama NCCR, mrema, UDP pia tuliwasikia wakati wa uchaguzi. Imani ya mtu huwa haibadiliki badiliki kama kinyonga. Ukiona mtu anabadilika badilika katika siasa, huyo hana imani yoyote. Lolote linalokuja kwake ni sawa tu. Hana msimamo.

    Kwa hiyo CHADEMA jipangeni kuingia vizuri. Wasipowaunga mkono kwa vile mmewakataa tutawaona. sio mara ya kwanza, wameshatuonyesha. Sisi tutasikiliza hoja zenu, hata zisiposikilizwa na kuungwa mkono, tutakuwa tumewajua wanaotutetea au kutukandamiza.

    Hata hivyo hata wakiwaunga mkono bado hamuwezi kuwazidi wabunge wa CCM. Maana wabunge wa CCM wanamtii rais wao hata kama wananchi wanaumia. Kwao bado "Zidumu fikra za mwenyekiti wa CCM". Utashangaa tunasikia kuna wapambanaji lakini wakiambiwa mguu sawa, wooote wananyoooooka sawa. Hakuna wa kukohoa. Wakiwa wao kwa wao tunasikia kuna makundi, ila likija suala la kitaifa wao hujificha nyuso zao, haoooooo, ili vitumbua vyao visiingie mchanga.

    Wachangiaji tafakarini maana haya mnayosema ndio yanaota mizizi kwenye mioyo yenu. Ukitetea unafiki, unakuwa mnafiki. Ukimuonea haya fisadi, wewe ndio unakuwa fisadi. Chagueni moja, kuwa wakweli au waongo.

    ReplyDelete
  18. Mnaita wenzenu wanafiki kwa kuunda serikali ya umoja hivi mnafikiri nyie peke yenu mnaweza kutawala dola ikiwa kila uchaguzi mnagawana kura za upinzani? Na kama hamuaminiani sasa huko mbele mtaaminiana?

    Kwanza tukianza kutafuta wanafiki hapa kati ya CUF na Chadema nani mnafiki? Ni CUF waliosimama kidete wakahakikisha wanawakilisha nusu ya wazanzibari kwenye serikali au ni Chadema ambao hata pesa za uchaguzi milioni 200 walipewa na kada wa CCM na hivi tena walipewa milioni 150 nyingine?

    Wanachoogopa Chadema kiwazi wao ni mamluki wako kwa ajili ya pesa tofauti na CUF ambao hawawezi kuchukua pesa kutoka CCM. Habari ndio hiyo, na subirini hao Chadema watakavyosambaratisha upinzani bungeni, na nafikiri sasa hivi Dr Slaa anajuta kwanini hakurudi bungeni akasikiliza maneno ya Mbowe. Na nyie mnaomtetea hamjui mlisemalo wacheni watu wanyamaze wasijesema mambo ambayo mtashindwa kuelewa kama kuna siasa Tz au ni biashara tu.

    ReplyDelete
  19. ewe mtanzania mwenzangu hii ni sehemu ya maoni siyo sehem ya kutukana au kutoa ghadhabu zako kwa viongozi wa aina yeyote awe wa upinzani au chama tawala kutukana hakuleti maana tunajua watanzania tulio wengi midomo nimaliyetu kuongea kwingi vitendo hakuna wenzetu wazungu husema mtumwenyetabia hiyo hulinganisha na akina dada ndio wanapigasana kelele vilevile tabia ya kutukana huonyesha upeo wako mdogo na elimu huna ya darasani na ya malezi umeambiwa uchangie mada changia sio kikwete au slaa sijui mboe au hamad rashid hata akiwa waziri yeye si yeye na familia yake kwa upeo wako ninani kiongozi atakae chaguliwa hapa atakupa wewe na familia yako unafuu wa maisha?ndugu zangu hangaika mwenyewe ujikomboe hakuna wa kukubba wewe jibebe mwenyewe chokochoko za nn?haomnao washabikia pakinuka hapo bongo msala mnabaki nao wenyewe wenzenu hawatakuwepo

    ReplyDelete
  20. Ukweli uwe unasemwa jamani hata kama mtu ana kwikwi ya kuona atamchafua mtu, kama anataka kuchafuliwa na haangalii na kuogopa asichafuliwe basi yabidi kuchafuliwa. Haya makanisa yoote kabisa yako upande wa Chadema. Mimi ni m-Kristu Katoliki safi sana. Lakini Maaskofu na wengine wa makanisa wanatishia watu maisha eti watatoa laana. Kuna laana nyingine ni batili hata mbele ya Mwenyezi Mungu. Wao walimpika Slaa kwenye sufuria lenye mafuta safi sana wakiwa na matumaini atatawala. Wakasahau Dimplomacy wakatanguliza udini wao wa ki-kristu bila ya kujali kwamba Mungu ni yule yule kwa dini zote. Ndio wanao mpa kiburi na majigambo huyo Slaa na wenzie, tukubali tusikubali. Hivi wao ni wachunga kondoo wa Mungu au ni wanasiasa. Tena hii issue ya kumpika Slaa kwenye masufuria wameanza miaka mingi sana. Sasa basi Slaa kakosa, visasi, maombezi, na kufuru waweke banki wasubiri 2015 kwani wanatuletea ugomvi kwenye mitaa na nchi nzima. Wapenda haki tutahamia kwenye uislamu maana tunaona Ukiristu hautendi haki na unachangia maovu. Ni kweli mapadre na maaskofu wavue kanzu wavae mashati waingie kwenye ulingo wa siasa tujue moja, tumechoka na kero zao za uchochezi.

    ReplyDelete
  21. JAMANI WA TZ TUNAKWENDA WAPI LAKINI MTUYUKO TAYARI KUANDIKA UUONGO COZ YA USHABIK WA CHAMA! UNAJIJUA ULIYEANDIKA UONGO SINAHAJA YA KUKUTAJA KUMBUKEN HAPATUNA ZUNGUMZIA MADA YA KAMBIYA UPINZANI HIZI ZA SLAA, KIKWETE, KUPOKEA MSAADA KWA KADA WA CCM NA UDINI VINATOKA WAPI! KUMBUKA HAKUNA VITA MBAYA KAMA YAUDI IKIANZA HAIISHI COZ KILAMTU ATASIMAMIA DINI YAKE KUWAMWANGALIFU USIJA UKAWA CHANZO COZ YAUSHABIK! ILIKUWA ANGALIZO TU TUJE KWENYE MADA, Tafadhali tuwewaangalifu kwenye kutoa maoni kumbuka nikwa manufaa ya taifaletu na sio ung'ang'anie kusafisha chamachako, toa maoni yatakayowasaidia chadema kufanya maamuzi sahii, kumbukeni wakati wakufungua bunge chadema kilitaka kuwshirikisaha ila CUf wakagoma pia wapinzani wakati ule hawakuwa upande wao walijiunga na CCM mfanomzuzi chaguzi zilizofanyika, nahata sikuile walipotoka nje wapinzani walikuwa wakwanza kujazia nafasi walizoacha. sasa iwaje leo wanapoonyesha wasiwasi na hao CUF ilihali wao zenj sio wapinzani? muwaponde kama siyo ushabiki wavyama? chamuhimu tungetoa maoni yatakayo wasaidia kuwashirikisha wenzao bila kuaribu umakini wa kambi. mfano mie nawapa njia mbili kama kwa CUF haiwezekani basi wawashirikishe kina NCCR na wenzie afu hao CUF wawemo kama washauri ila wasiwape uwaziri ila waakikishe kuwa wanapokea hojazao na mashauri yao coz nikweli itakapo tokea isue inausu muunganiko wa zanzibar itakuwashida kwao kusimama kama wapinzani, sjui kamahilo linawezekana coz sjui kanuni zinaendaje. njia ya pili wawashirikishe wote ila kawe na masharti makali yeyote atakaye wasaliti wenzie anatolewa papokwapapo ndani ya masaa 24 nazani chadema hili linawezekana coz nyiendo viongoz sio pliz zimebaki sikuchahe naomba mtoe maamuzi sahii msije aribi CV yenu naamini siyo kuwa hamtaki coz mlionyeshania toka mwanzo bur tatizo ni kuaminiana. nakwaupande wetu wananchi tubadilike tuache ushabiki usiokuwa na manufaa na maisha yetu, tutoe mawazo yenye tija watu wanatoa maoni nje ya mada utafikiri hawajasoma madainahusu nini! jamani watz ifike mahali tuchague viongoz kutokana nuutendaji wao na siyo anatoka chamagani ifike mahali kwenyejimbolako unachagua rais chama kingine diwani kingine na mbunge kingine, ifike mahalituwajengee mazingira viongoziwetu wawe wabunifu wafanye nini ili wasije wakatoswa uchaguzi unao fuata, ifike mahali chama kitawale miaka 50 kutokana na uwajibikaji na maendeleo na siyo sababa tunakipenda, Hata hawa chadema kamawatashika dola wakitubadilikia tunamtoa huyo slaa baada ya miaka 5 hatusubiri hata amalize 10 tunajaribu kwingine hakika tukifanya hivi mtaona watakavyo wajibika na umaskin tutauweka kwenye vitabu vyahistoria iliwajifunze watotowetu tulikotoka; mie nnauhakika 100% lait Dr Slaa angegombea kwa tiketi ya CCM na sea zake hizi hizi angeshinda kwa asilimia zaidi ya 90% ila sababu tumejijengea Rais lazima atoke CCM hata ikifika maali wakamsimamisha mtu asiye na akili timamu tutamchagua ndomana kikwete alisema CCM itatawala milee!

    TAFAKARI, CHUKUA HATUA

    ReplyDelete
  22. Uchaguzi uliopita umetoa maamuzi:
    1. CCM imetangazwa kushinda na kuunda serikali
    2. CHADEMA imepata wabunge wa kutosha kuunda serikali kivuli

    Huo ndio uamuzi wa wananchi.
    CCM wanajiamini na wameunda serikali kama kawaida yao.
    CHADEMA nao wameunda serikali kivuli, ingawa inaonekana hawajiamini sana, sijui ni kwa vile ni mara yao ya kwanza, au hawakutegemea sijui. Hawataki kuonyesha msimamo.

    CCM walikubaliana na CUF kutawala pamoja zanzibar. na ndivyo walivyofanya. kwa bara hapana.

    CHADEMA je, mlikubaliana kuunda serikali kivuli na CUF, NCCR-mageuzi, TLP au UDP? Kama ndio msiwaasi wenzenu. Kama jibu ni hapana, mjiamini mtuambie kwa kujiamini sio kila siku tunasikia mkiwaambia wenzenu wasubiri. Au mkitaka kulipa fadhila za CUF miaka ya nyuma, lipeni tu fadhila ili muwe miongoni mwa mafisadi. Maana mafisadi hulipa fadhila kwa waliowachangia hela kwenye uchaguzi na kuwasahau waliowachagua.

    Kumbukeni CUF hawakuwa na uhalali wa kuunda upinzani wao wenyewe. Kwa hiyo vyama vyote vilivyoshiriki kwenye upinzani vilikuwa na haki. Haikuwa favour!

    Tuache hivi vyama viwili viunde serikali zao. Sisi wengine tushiriki kama wawakilishi wa wananchi tu.

    Kila chama kina sera zake jamani, tusijidanganye. Kila chama ni mpinzani wa mwenzake. La sivyo tunge kuwa na vyama vichache. Kila chama kifanye bidii kupata hizi nafasi kwenye uchguzi ujao. Uchaguzi ujao kila chama kitawania upya kuunda serikali, au kuunda upinzani. Kazi kwenu. msipoweza basi msubiri tena. Mbona hawa wanaotaka upinzani bungeni hawawasumbui CCM kuomba watawale pamoja kama Zanzibar?

    ReplyDelete
  23. Tuache ushabiki wa kidini. Sina hakika mwenzetu ana % gani kuhusisha Chadema na Kanisa Katoliki. Ni vema tukitoa maoni yenye kuhimiza umoja na si kuchochea difference. Chadema na CUF kuungana naona ni jambo gumu. Umoja wa Kitaifa ZBR tuliutafuta -jambo jema. Kiasi gani CUF kushikamana na Chadema kudai mambo ambayo CUF inanufaika nayo kwenye Umoja wa Kitaifa ni kitendawili/party loyalty. Lililo tete ni dai la kurekebisha KATIBA ya MUUNGANO ambayo hadi sasa INAMNYIMA MBARA HAKI YA YA UTANGANYIKA na masuala mengine ya uwakilisi. Hili linataka mshikamano wa kitaifa baina ya wapinzani Bungeni...nahisi halitaweza kupata msukumo toka kwa CUF -ZBR Bungeni. Ikiwa ndio hivyo TLP, UDP, NCCR-M na CUF-Mwakilishi toka BARA watakuwa wapi? Tukubaliane tusikubaliane hili si jambo ni gumu.

    ReplyDelete
  24. Hivi nyie Cuf sisi Wazanzibar ndio wapiga kura wenu,je tuliwatuma kuwa lazima muungane na Chadema kwenye kambi ya upinzani? sisi tumechagua CUF kutuwakilisha sio kambi ya upinzani,kaeni wenyewe,huyo Mbowe ni mfanyabiashara mwenye malengo binafsi na siasa iko tofauti na yeye kama yalivyotofautina macho yake,sisi wana CUF tumewatuma mtuwakilishe huko bungeni kama CUF na wengi wetu hatuijui kambi hiyo zaidi ya CUF, UMOJA WA KITAIFA NI BORA KWETU KULIKO HIYO KAMBI NA TUJIPANGE SASA KUJIKOMBOA KWENYE MAKUCHA HAYA YALIYOIRUDISHA NYUMA ZANZIBAR.

    ReplyDelete