26 January 2011

Chuo Kikuu Makumira watawanywa kwa mabomu

Na Glory Mhiliwa, Arusha

ASKARI wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) jana walitumia mabomu ya machozi kusitisha maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha
Tumaini (Makumira) ambao waliokuwa wakiandamana kushinikiza serikali kuwapatia mikopo kupitia Bodi ya Mikopo.

Maandamano hayo yalianza jana saa 3:00 asubuhi ambapo wanafunzi hao walikuwa wakiandamana ili kushinikiza Bodi ya Mikopo kuwapatia fedha zao kama walivyoahidi tangu mwaka jana.

Katika tafrani hiyo baadhi ya wanafunzi walijeruhiwa na wengine kukamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Usa River, Arumeru.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya maandamano yao kutawanywa, wanafunzi hao walisema;

"Hapa unavyotuona hatujala wengine leo siku ya pili hatuna hela hata sh. kumi. Darasani tunaingia lakini hatuna hela ya kununua vitabu na vifaa vingine muhimu vya shule, sisi tunataka tujue kama Bodi ya Mikopo haijatoa fedha ama ni uongozi wa chuo ndio uliochakachua fedha zetu," alisema mwanafunzi mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Bw. Alphonce Mallya.

Alisema kuwa bodi ya mikopo hivi karibuni ilitoa fedha lakini kwa baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa pili na mwaka wa tatu, lakini wa mwaka wa kwanza ambao wapo kama 700 hawajapatia mikopo.

"Wengine sisi wanawake inabidi tukajiuze ili tupate hela ya kujikimu, njaa ni mbaya sana ikiuma utafanya chochote. Sasa wenzetu wanaume sijui wakajiuze wapi, tunafanya hivi kwa kukosa fedha. Bodi ya Mikopo imetuahidi lakini mpaka sasa haijatupatia fedha hizo," alisema mwanafunzi mwingine ambaye hakupenda kutaja jina lake.

Walidai kuwa mwanafunzi mmoja ambaye ni yatima wa mwaka wa kwanza, Salome Samburu, hivi sasa amelazwa hospitali ya Selian akipatiwa matibabu baada ya jana kuzirai baada ya jina lake kukosekana kwenye orodha ya wanafunzi  wanaotakiwa kulipiwa na bodi ya mikopo, wakati awali jina lake kuonekana kwenye mtandao.

"Hapa hatuna hela lakini tumejichangisha sh. 100,000 na kumkimbiza mwenzetu hospitalini akatibiwe. Ni yatima, hana hata sh. moja, alipokosa jina lake alizimia hapohapo," alisema Bw. Mallya

Wanafunzi hao walidai kuwa wote wanaostahili kupata mikopo wameshasaini mkataba na bodi hiyo lakini cha kushangaza hawajapatiwa.

"Jamani sisi hapa wote tunadai kama milioni 200 hivi wanafunzi lakini serikali inatudharau sisi na kukubali kuilipa dowans  mabilioni ya fedha wakati tumeambiwa hatutafanya mtihani mwezi ujao kama tutakuwa hatujalipa," alisema Devis Thobias.

Mkuu wa Chuo cha Makumira, Prof Joseph Parsalaw alisema kuwa anashangazwa na hatua ya wanafunzi hao kufanya fujo wakidai mikopo yao wakati uongozi wa chuo na serikali ya wanafunzi wameshakaa kwa ajili ya kupata ufumbuzi.

"Sisi hatutoi mikopo, wanaotoa ni bodi sana sana tunawasaidia wapate mikopo yao, sasa siyo kweli wanavyosema kuwa uongozi wa chuo ndio unashikilia fedha zao fedha zao, bado hazijatumwa na bodi ya mikopo," alisema Pfor Parsalaw.

Alisema kuwa inawezekana wanafunzi hao wameamua kuandamana baada ya kuona wenzao wa vyuo vingine wakiandamana, lakini chuo hicho hakikuwa na historia ya wanafunzi kuandamana hovyo.

Alisema kuwa uongozi wa chuo ulimtuma Rais wa Serikali ya Wanafunzi kwenda kwenye bodi ya mikopo kufuatilia na alirudi juzi, ambapo baadhi ya wanafunzi fedha zao zililetwa na wengine zikaendelea kuchelewa.

No comments:

Post a Comment