LONDON, Uingereza
ARSENAL imefuzu fainali ya Kombe la Ligi, baada ya kuichapa Ipswich mabao 3-0 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa Uwanja wa Emirates usiku wa
kumkia jana.
Kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger amefurahi na kusema kama watatwaa ubingwa huo itawaongezea ari wachezaji wake na kuwafurahisha mashabiki.
Miamba hiyo ya Emirates, ililazimika kusubiri hadi dakika 30 za mwisho kuweza kupata magoli ambayo yataifanya kucheza fainali kwenye Uwanja wa Wembley na kufufua matumaini ya kuanza kupata kombe msimu huu.
Arsenal ilipata mabao mawili ya haraka kupitia kwa Nicklas Bendtner na Laurent Koscielny na kisha kupata bao jingine lililowekwa kimiani na Cesc Fabregas, ikiwa zimesalia dakika 13 na kufanya Gunners kusonga mbele kwa uwiano wa mabao 3-1.
Katika fainali itakayochezwa Uwanja wa Wembley Februari 27, mwaka huu Arsenal watakutana na Birmingham City au West Ham United.
Arsenal ililazimika kujituma ili kuibuka na ushindi, baada ya kufungwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa katika Uwanja wa Portman Road, hadi zilipobaki dakika 15 kipindi cha pili walikuwa bado wako nyuma.
Ipswich ambayo inacheza Ligi Daraja la Kwanza ilicheza kwa kujituma, lakini mshambuliaji wa Denmark, Bendtner ambaye amekuwa akihusishwa na habari za kuondoka katika klabu hiyo katika kipindi cha usajili mdogo mwezi huu, alifunga bao dakika 61, baada ya kupasiwa mpira mrefu na akamfunga kipa, Marton Fulop.
Mlinzi wa Kifaransa, Laurent Koscielny alifunga bao jingine dakika tatu baadaye na kuifanya Arsenal kuwa mbele kwa mabao 2-0 na uwiano kuwa mabao 2-1 .
Mchezaji Jason Scotland alipata nafasi nzuri kuisawazishia Ipswich, lakini shuti lake liliokolewa na Wojciech Szczesny, kabla ya nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas kufunga bao jingine dakika ya 77 akitumia vyema pasi kutoka kwa Andrei Arshavin.
Akizungumzia ushindi huo kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alisema hii inaweza kutufanya kupata kombe la kwanza kati ya mengi msimu huu.
“Tunajaribu kushinda kila kitu tunachoweza. Kama tunaweza kushinda hili itakuwa ni presha ya kushinda katika mashindano mengine,” alisema.
Alisema msimu huu malengo yao ni kutwaa makombe na kama watafanikiwa hilo wanaweza kufikia malengo mengine.Arsenal haijatwaa kombe katika misimu mitano mfululizo. Katika msimu huu iko katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, hivyo kuwa miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kutwaa ubingwa pia imo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wachezaji wa timu hiyo, pamoja na mashabiki wamekuwa na hamu kubwa ya kuona timu yao ikitwaa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu England pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambalo hawajawahi kulitwaa pamoja na kufika fainali.
Timu hiyo imekuwa ikitumia wachezaji vijana.
No comments:
Post a Comment