05 January 2011

Mtibwa Sugar yatinga robo fainali kombe la Uhai

Na Addolph Bruno

TIMU ya soka ya vijana wenye miaka chini ya miaka 20 ya Mtibwa Sugar, imekata tiketi ya kucheza robo fainali ya Kombe la Uhai, baada ya kuichapa Kagera Sugar
mabao 2-0.

Mchezo huo wa Kundi C ulichezwa jana, katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.


Mtibwa iliwachukua dakika 10, kupata bao la kwanza kupitia kwa Issa Rashidi 'Baba Ubaya', baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kudaka kipa wa Kagera Sugar,  Hassan Boshen.

Bao hilo liliwafanya Kagera Sugar kuja juu na kuliandama lango la wapinzani wao, lakini washambuliaji wake walishindwa kutikisa nyavu za wapinzani wao.

Kagera walipata nafasi nzuri dakika ya 20 na 38, lakini mabeki wa Mtibwa walikuwa makini kuondosha hatari langoni kwao.

Mtibwa Sugar ilijipatia bao la pili dakika ya 83, kupitia kwa Michael Mgimwa, aliyepiga mpira uliojaa moja kwa moja wavuni.

Mtibwa inakuwa ni timu ya kwanza kutinga robo fainali  katika kundi lao, ikitanguliwa na timu za AFC Arusha na  Ruvu Shooting kundi A, Simba na Yanga, kundi B huku hatua ya makundi ya michuano hiyo ikimalizika jana jioni kwa mchezo kati ya Majimaji FC dhidi ya JKT Ruvu na mshindi kuingia robo fainali.

No comments:

Post a Comment