Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo wa Temeke, Abbas Mtemvu ametoa sh. 500,000 kwa ajili ya taasisi ya Keko Mwanga Development Foundation (KEMWADEFO), zitakazotumika kuendesha mashindano ya kumuenzi muasisi wa michezo katika
Kata ya Keko, Dar es Salaam Miraji Salum 'Kizoka'.
Akizungumza katika uzinduzi wa mashindano hayo kwenye viwanja vya Sigara, Dar es Salaam juzi, Mtemvu alisema michezo ndiyo njia ya pekee ya kuwafanya vijana kuepuka vishawishi na kujenga miili yao.
Katika uzinduzi wa mashindano hayo ambayo yatashirikisha timu 10 za Keko Mwanga, timu ya Veterani ya KEMWADEFO ilifungwa mabao 4-0 na timu ya Waandishi wa habari za Michezo (TASWA).
Mbali ya jitihada za mabeki wa KEMWADEFO, Francis Julius, Henry Nindi na Rashid Kamanyola kujitahidi kuwalinda washambuliaji wa TASWA ilijikuta inafungwa la kwanza na Mohamed Akida, dakika ya tisa baada ya kupokea pasi ndefu ya Sultani Sikilo.
Bao la pili la TASWA, lilifungwa na Julius Kihamba dakika ya 23 aliyeunganisha pasi ya Majuto Omari na bao la tatu lilifungwa na Kihampa tena kabla ya Majuto kufunga bao la nne dakika ya 54.
Mechi ya kwanza ya ufunguzi wa mashindano hayo, ilizikutanisha timu za Eleven Fighter na Bad Boys katika pambano kali lililokuwa kivutio kwa mashabiki wa soka waliohudhuria.
Pamoja ya ufundi wa kusakata soka ulioneshwa na timu hizo, Eleven Fighter ilishinda mabao 2-0 huku bao la kwanza likifungwa na Dini Dadi dakika ya 26 kwa mpira wa adhabu na bao la pili lilifungwa na Salum Taratibu dakika ya 70 aliyeunganisha pasi ya Januari Augustino.
No comments:
Post a Comment