18 January 2011

Tenga kupasua jipu la waamuzi wa FIFA

Na Zahoro Mlanzi

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga leo anatarajia kukata mzizi wa fitina kwa kuelezea kilichojiri katika sakata la waamuzi waliopewa beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kinyume na
taratibu.

Shirikisho hilo liliingia katika kashfa hiyo, baada ya kudaiwa kupeleka majina ya waamuzi tofauti na yale yaliyowasilishwa na Kamati ya Waamuzi nchini huku yaliyostahili yakikatwa.

Waamuzi wanaodaiwa kuingizwa na TFF kinyemela ni Oden Mbaga, Hamis Chang'walu, Jesse Erasmo na Israel Nkongo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura wakati akitangaza waamuzi watakaocheza michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, alisema Rais Tenga atalitolea ufafanuzi suala hilo leo.

"Siwezi kulizungumzia suala hilo ila hilo ni moja ya ajenda ya Rais Tenga atakapozungumza na vyombo vya habari kesho (leo), kila kitu kitakuwa wazi lakini CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika) ndiyo waliowachagua si sisi," alisema Wambura.

Wambura aliwataja waamuzi watakaochezesha michuano hiyo kuwa Waziri Sheha, Kombo Ali na Samuel Mpenzu ambao watachezesha mchezo wa Kombe la Shirikisho kati ya SOFAPAKA ya Kenya dhidi ya AS Aviacao ya Angola, utakaopigwa kati ya Februali 11, 12 na 13 nchini Kenya.

Alisema Waamuzi Mbaga, Chang'walu na John Kanyenye watachezesha mechi ya Klabu Bingwa Afrika kati ya Young Buffaloes ya Swaziland na St. Michael United ya Shelisheli na Hafidh Ali ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi ya Klabu Bingwa Afrika kati ya ZESCO United ya Zambia na Desportiva Muculmana ya Msumbiji.

Wambura aliongeza kuwa waamuzi Ramadhan Kibo na Nkongo wameteuliwa kuwa waamuzi wa akiba kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya KMKM ya Zanzibar na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

No comments:

Post a Comment