LONDON, England
KOCHA wa Everton, David Moyes amesema kuwa wamepokea ofa kutoka kwa Chelsea kuhusu kiungo wao, Steven Pienaar ikiwa ni baada ya kukataa ofa kutoka kwa Tottenham.Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, raia wa
Afrika Kusini alikuwa nje ya kikosi kilichotoka sare ya mabao 2-2 na Liverpool Jumapili iliyopita na Moyes, alikaririwa akisema kichwa chake kilikuwa si kizuri kwa kucheza.
Pienaar anatarajiwa kuwa nje ya mkataba mwishoni mwa msimu huu na Chelsea inasadikika kurusha ndoana ya pauni milioni 3, ili kumnasa mchezaji huyo.
Mchezaji huyo wa zamani wa Ajax alijiunga na Everton mwaka 2007 akitokea Borussia Dortmund kwa kitita cha pauni milioni 2.
"Pienaar bado hajafikia makubaliano na Chelsea," alisema Moyes. "Ila tumeshamkabidhi mwakilishi wa kufanya mazungumzo na Chelsea. "Ila hatukumruhusu kufanya mazungumzo na Tottenham kwa sababu hawakutoa kiasi cha fedha kama hicho," aliongeza na akasema endapo Tottenham watatia kiasi kama hicho, wanaweza kubadili msimamo vinginevyo wataingia makubaliano na Chelsea.
Hata hivyo akizungumza baada ya timu yake kutoka sare ya mabao 2-2 na Manchester United, kocha wa Spurs, Harry Redknapp alieleza kuwa klabu hiyo ya White Hart Lane inavyoelekea haina mpango wa kutoa kiasi kama cha Chelsea kwa ajili ya nyota huyo wa Afrika Kusini.
Msimu uliopita, Pienaar alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa klabu lakini msimu huu hakuweza kufikia kwenye kiwango kama cha mwaka jana na mapema msimu huu, Moyes alisema kuwa mchezaji huyo amekataa kusaini mkataba mpya.
No comments:
Post a Comment